Na Mwandishi wetu, Mbulu
Aliyekuwa mbunge wa Mbulu vijijini mkoani Manyara, Flatey Massay kwa tiketi ya CCM kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo tangu mwaka 2015 hadi 2025 ambaye jina lake lilikatwa hivi karibuni baada ya kuchukua fomu ya CCM, amejiunga na chama cha ACT Wazalendo na kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Massay ambaye aliweka histori ya kuruka sarakasi bungeni wakati akiomba barabara ya laki ya Karatu – Mbulu – Haydom hadi Lalago mkoani Simiyu, jina lake lilikatwa na kamati kuu ya CCM.
Mgombea huyo wa ACT Wazalendo amekabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo na msimamizi msaidizi wa uchaguzi jimbo la Mbulu vijijini Joseph Sambo.
Baadhi ya wanachama wa ACT- Wazalendo walimsindikiza mgombea wao hadi kwenye ofisi za msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Sambo.
Massay baada ya kukabidhi barua ya utambulisho wa ACT Wazalendo kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa jimbo hilo alikabidhiwa fomu ya kuomba uteuzi wa nafasi hiyo.
Msimamizi msaidizi huyo Sambo ameeleza kwamba siku ya mwisho ya kurejesha fomu hiyo baada ya kuijaza ni Agosti 27 mwaka 2025.
Awali, Massay alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM Julai 28 mwaka 2025 ila jina lake na waliokuwa wabunge wawili Christopher Ole Sendeka (Simanjiro) na Pauline Gekul (Babati mjini) yakakatwa na kamati kuu ya CCM.
Hata hivyo, majina matano ya Bahati Sulle, Grace Saulo, Festo Bayo, Dk Emmanuel Nuwas na Samwel Malleyeki yakarudishwa.
Katika uchaguzi uliofanyika Agosti 4 mwaka 2025 Bayo aliongoza kwa kura 5,706, Dk Nuwas kura 3,168 Grace 1,484 Sulle 149 na Malleyeki 127 ila Agosti 23 mwaka 2025 jina la Dk Nuwas likapitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho.