Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnson Johansen Mutasingwa, ameweka wazi dhamira yake ya kuliongoza jimbo hilo kwa mshikamano na ushirikiano, akisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kupatikana pasipo umoja wa wanachama na wananchi kwa ujumla. Alitoa kauli hiyo baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge katika ofisi za Manispaa ya Bukoba, ambapo alisisitiza kuwa huu si ushindi wake binafsi bali ni wa chama kizima.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mutasingwa aliwataka wanachama wa CCM kuachana na makundi ya ndani ya chama, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha jitihada za pamoja za kuleta maendeleo. Alisisitiza kuwa mshikamano ndio silaha muhimu ya ushindi wa chama hicho katika uchaguzi ujao, na akatoa wito kwa kila mmoja kuchangia kampeni kwa njia chanya na ya mshikamano.
Mhandisi huyo pia aliwashukuru wananchi waliomsindikiza kuchukua fomu na kuonyesha imani kwake, pamoja na uongozi wa chama kwa kumchagua kupeperusha bendera ya CCM. Aliahidi kuwa, akichaguliwa, atahakikisha anawatumikia wananchi wote wa Bukoba Mjini bila ubaguzi, kwa kuzingatia kuwa maendeleo hayana itikadi za kisiasa, bali yanahitaji dhamira ya kweli ya kuhudumia umma.
Kwa upande mwingine, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Melkion Komba, alithibitisha kuwa mgombea huyo amekidhi vigezo vyote vya kisheria na kupewa barua rasmi ya kugombea. Alimtaka kuhakikisha anajaza na kurejesha fomu kwa wakati kabla ya tarehe ya mwisho ya Agosti 27, 2025, kama ratiba ya uchaguzi inavyoelekeza.