Korogwe, Tanga
Vikundi vya kijamii vinavyoshiriki katika matengenezo madogomadogo ya barabara wilayani Korogwe, mkoani Tanga, vimepongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa Uboreshaji na Ufunguaji wa Fursa za Kiuchumi na Kijamii Vijijini (RISE), ambao utasaidia kuimarisha miundombinu ya barabara na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Mradi huo unatekelezwa na serikali kupitia Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ambapo awamu ya kwanza imeanza katika mikoa minne kwenye halmashauri nane.
Akizungumza wakati wa mafunzo elekezi kwa vikundi hivyo yaliyotolewa na TARURA, Bw. Hassan Mshauri kutoka Kikundi cha Mchanganyiko amesema mafunzo hayo yamewapa ujuzi wa kuhakikisha barabara katika maeneo yao zinabaki kupitika wakati wote.
“Mafunzo haya tumeyapata bure na yametupa mbinu za kujikimu kimaisha kupitia ujuzi tuliojifunza. Pia sisi tutakuwa walimu wa baadae kwa kuwafundisha wenzetu namna ya kushiriki katika matengenezo madogo ya barabara ili kujikwamua kimaisha,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Uvumilivu, Bi. Maria Simoni, amesema hatua ya serikali kuwezesha mafunzo hayo itawapa hamasa ya kutunza barabara kwenye maeneo yao.
“Tukitoka hapa tutahakikisha barabara za vijijini zinadumu kwa muda mrefu bila mashimo wala mifereji kujaa taka. Tunaishukuru TARURA kwa kutupa elimu hii bure bila gharama,” amesema.