Chama Cha Mapinduzi CCM, kimehitimisha mchakato wa uteuzi wa wagombea wake wa ubunge kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ambapo matokeo yake yameibua mshangao baada ya baadhi ya majina makubwa kuachwa nje na sura mpya kuteuliwa.
Katika mabadiliko hayo, Msanii wa muziki anayefahamika kwa jina la Baba Levo (Clayton Revocatus Chipando) naye ameteuliwa katika Jimbo la Kigoma Mjini. Hii ni baada ya kumaliza wa pili kwenye kura za maoni nyuma ya mbunge anayemaliza muda wake, Kirumbe Ng’enda.
Lakini miongoni mwa waliokosa nafasi ni Ummy Mwalimu, aliyewahi kuwa Waziri wa Afya. Hata baada ya kuongoza kura za maoni kwa kura 5,750 katika Jimbo la Tanga Mjini, jina lake limekatwa na nafasi yake kuchukuliwa na Omary Ahmed Ayoub.
Aidha, wanasiasa waliokuwa wapinzani na maarufu kama wabunge wa zamani wa Chadema, Esther Matiko na Esther Bulaya, wamerejea kupitia CCM. Matiko ameteuliwa kugombea Jimbo la Tarime Mjini, huku Bulaya akiwania tena Jimbo la Bunda Mjini, licha ya kushika nafasi ya tatu kwenye kura za maoni.