Na. Mwandishi Wetu – MAELEZO, Mbeya
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amesema uandishi wa Habari na utangazaji ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine nchini akisisitza kuwa mtu yeyote anayetaka kutekeleza majukumu yanayohusiana na tasnia hiyo nchini Tanzania, lazima awe na elimu na vigezo vinavyotakiwa.
Prof. Kabudi amesema hayo Agosti 18, 2025 Jijini Mbeya alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa wadau wa Habari na Utangazaji kutoka Mikoa ya nyanda za juu kusini wa kujenga uelewa wa pamoja kwa pande zote ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.
“Nalisema hili kwa uchungu sana, watu waliamini kuwa kuwa mwandishi wa Habari au mtangazaji ni kipaji na sio taaluma jambo ambalo sio kweli, uandishi wa Habari ni taaluma ambayo ina vigezo vya kufuata na maadili ya kuzingatia. Uandishi wa Habari ni taaluma nzuri, ni lazima tuijali” amesema Prof. Kabudi
Prof. Kabudi ametoa wito kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakitekeleza majukumu ya kihabari bila kuwa na vigezo vya kitaaluma wajiendeleze ili waweze kupata ithibati akibainisha kuwa Serikali imeanzisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ili kulinda taaluma ya habari ambapo bodi hiyo imeingia makubaliano na vyuo vinavyotoa taaluma ya habari kikiwemo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ili kuwezesha wanahabari kusoma.
Katika hatua nyingine Waziri Kabudi ametoa wito kwa waandishi wa habari wazingatie weledi na kuwa wazalendo kwa nchi kutokana na umuhimu wao katika kulinda na kuhamasisha wananchi kuilinda na kuitetea na kuipenda nchi.
“Mwandishi wa habari unapokuwa mzalendo kwa kuipenda, kuienzi na kuithamini nchi yako haimaniishi kwamba haina changamoto na haina maana kuwa ndani ya nchi hakuna yaliyopungua la hasha ni kwa sababu unajua hiyo ndiyo nchi yako, mahali ulipozaliwa na mahali unapoishi” amesisitiza.
Amewataka waandishi wa habari waendelee kuzingatia taaluma kwa kuwa yapo mataifa ambayo chaguzi zao huishia kwenye machafuko kutokana na wagombea wao kuamua kujitangazia matokeo ya uchaguzi nje ya utaratibu wa taasisi rasmi zilizowekwa kisheria kutangaza matokeo jambo ambalo limekuwa chanzo cha kuvuruga amani.