Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kufanya maboresho ya Sheria mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa Dira 2050, Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lkilchofanyika tarehe 18 Agosti, 2025 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza mkakati wa kufanya maboresho katika sheria ili kuhakikisha kuwa, sheria, sera, mipango, malengo na mikakati mbalimbali pamoja na vigezo na viashiria vilivyowekwa vya upimaji wa matokeo ya kiutendaji wa Watumishi wa umma, vinafungamanishwa na malengo na shabaha ya Dira ya 2050.
*”Ofisi yetu, inao wajibu wa kupanga, kuratibu, kutekeleza michakato ya tathmini na mapitio ya sheria za Bunge na sheria ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kufanya maboresho na marekebisho muhimu ili kuziwezesha Taasisi za Umma kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya 2050 kwa ufanisi na tija.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewaeleza Wajumbe wa Baraza hilo kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kutekeleza mpango kazi wake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa kuandaa Miswada mbalimbali ya Sheria 19, kutafsiri Sheria Kuu 433 kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili, kuandaa maazimio mawili ambayo yaliidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kukamilisha Urekebu wa Sheria Kuu 446 za nchi na kuandaa Toleo la Sheria zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023.
Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa jumla ya Mikataba 3,436 ya Kitaifa na Kimataifa na Hati za Makubaliano (Memorandum of Understanding) 729 zilifanyiwa upekuzi na takribani maombi 4,151 ya ushauri wa kisheria yalipokelewa na kufanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Wajumbe wa Baraza na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na misingi mikuu minne ambayo ni utaalamu/weledi, ubunifu, uadilifu na uwazi, ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika Dira na Dhima ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*”Maafisa na Watumishi wote tulio hapa, ni jukumu letu kuhakikisha Dhima ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatekelezwa ili kufikia Dira ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amesema kuwa Baraza hilo limekutana kwa lengo la kupitia mipango mbalimbali iliyotekelezwa, inayotekelezwa na inayotarajiwa kutekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*“Mhe. Mwenyekiti leo tumekutana kwa ajili ya kupitia mipango tuliyoiweka kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili iweze kushauriwa na pengine kupewa maelekezo mbalimbali ambayo ni muhimu kuzingatiwa, ikihusisha masuala yanayohusu Wafanyakazi na utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Zella Rwemanyila ameushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*“Chama cha Wafanyakazi TUGHE tunawapongeza viongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa jitihada zenu mnazozifanya na mnazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha kuwa mnaboresha mazingira ya kazi katika Ofisi yetu.”* Amesema Bi. Zella.