Kimataifa, Habari kwa hisani ya (BBC)
Rais wa Marekani wa , Donald Trump, amesema kuwa “hakuna makubaliano hadi pale kutakapokuwa na makubaliano”, licha ya mazungumzo yake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kuonyesha dalili za maendeleo juu ya suala la Ukraine.
Trump alitoa kauli hiyo baada ya kikao cha karibu saa tatu kilichofanyika Alaska, akieleza kwa waandishi wa habari kuwa “hatukufika huko”.
Kwa upande wake, Putin alisema kuwa ana nia ya dhati kumaliza mzozo wa Ukraine, ingawa hakutoa maelezo ya kina. Wawili hao hawakuchukua maswali kutoka kwa wanahabari waliokuwapo.
Katika mahojiano ya baadaye, Trump alimshauri Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky — ambaye hakualikwa kwenye mkutano huo wa kilele — “kufanya makubaliano” ili kumaliza vita.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema Trump, anayejitambulisha kama mpatanishi na mtaalamu wa makubaliano, ameondoka Alaska bila kupata matokeo ya moja kwa moja.
Awali, viongozi hao walionekana wakibadilishana salamu za kirafiki kwenye uwanja wa ndege wa Anchorage, ambapo walishikana mikono mara mbili na kisha kusafiri pamoja kwenye gari la kifahari la Trump kuelekea ukumbi wa mkutano.
Kwa upande wa Kyiv, wachambuzi kama Vitaliy Shevchenko wanasema wananchi wa Ukraine wamepumua kwa afueni baada ya kutojitokeza makubaliano yoyote ambayo yangeligharimu taifa hilo sehemu ya ardhi yake.