SELF Microfinance imeweza kujenga uwezo kwa taasisi 549 kwa kutoa ushauri mbalimbali, kukaa nazo na kuzisaidia namna ya kujiendesha.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa SELF Microfinance, Bi. Santieli Yona, akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri (TEF) na taasisi hiyo, kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square, jijini Dar es Salaam.
Amesema huduma za fedha bado ni eneo linalohitaji kuwekewa mkazo hasa katika kutoa elimu, kwa kuwa elimu hiyo haijafika kila mahali.
Bi. Yona amesema kuwa moja ya mafanikio waliyoyapata ni kutengeneza ajira. “Sisi tunatoa mikopo kwa taasisi zinazokopesha na pia kwa wajasiriamali. Wajasiriamali hawa wanapopewa fedha, wanajiajiri na kutoa fursa kwa watu wengine,” alisema.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki, wameweza kutoa ajira zipatazo 183,000, jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa taifa, kwani si serikali pekee inayoweza kutoa ajira, bali kila mmoja anaweza kujiajiri na kujikimu.
Aidha, mafanikio mengine ni kuanza kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni utekelezaji wa ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan. Amesema mikopo hiyo itakapowafikia wananchi, itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.
Pia, SELF Microfinance inatoa elimu ya fedha mara kwa mara kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo maonesho ya Nanenane, Sabasaba, makongamano na kupitia vyombo vya habari. “Nia ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata elimu ya fedha, kwa kuwa bado wengi hawajafikiwa,” alisema.
Bi. Yona ameongeza kuwa, wanapenda kufuatilia kuona kama huduma zao zinabadilisha maisha ya wanufaika. “Kila baada ya muda tunapenda kujua walikuwa wapi, mikopo imewasaidiaje, na wapo wapi sasa,” alisema.
Amefafanua kuwa mkopo unapotumiwa vizuri unaweza kukuza biashara, lakini usipotumiwa ipasavyo unaweza kusababisha matatizo. “Unapotumia mkopo vizuri, uwe na uhakika utakusaidia. Lakini ukitumia kinyume na malengo, au bila usimamizi mzuri, fedha hazitakusaidia na zinaweza kukuingiza kwenye matatizo zaidi,” alisema.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto, ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kukosa elimu ya fedha, kushindwa kufanya tathmini kabla ya kukopa, na hulka ya watu wachache kutojali kurejesha mikopo.
“Ni vizuri kabla ya kukopa ufanye tathmini ya kina kuhusu utumizi wa fedha hizo kwenye biashara yako. Ukijipanga vizuri, utakuwa na uhuru na kujiamini. Lakini ukishindwa kurejesha, inaleta changamoto kwa wakopeshaji na inaweza kuongeza gharama za mikopo,” alisema Bi. Yona.