Elimu ya madhara ya kujiunganishia umeme bila kufuata taratibu ikiendelea kutolewa na wataalamu kutoka TANESCO Jijini Mwanza.
Mdhibiti mapato wa TANESCO Mkoa wa Mwanza Mhandisi Rajabu Marwa (kushoto)akitoa elimu kwa baadhi ya wananchi.
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mwanza limeanza oparesheni maalum ya kuwasaka na kuwachukulia hatua kali watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umeme pamoja na wizi wa nishati hiyo.
Akizungumza leo jijini Mwanza, Mdhibiti Mapato wa TANESCO Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Rajabu Marwa, amesema oparesheni hiyo inalenga pia kukomesha vitendo vya wananchi kujiunganishia umeme kinyume cha taratibu kwa kutumia mafundi wasio rasmi maarufu kama vishoka.
“Tumejipanga kuhakikisha kila atakayebainika kufanya vitendo vya hujuma na wizi wa umeme anachukuliwa hatua kali za kisheria. Hii ni sehemu ya jitihada zetu kudhibiti uchumi wa taifa na kulinda miundombinu ya umeme ambayo ni mali ya Watanzania wote,” amesema Mhandisi Marwa.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia huduma rasmi ya Nikonekt ya TANESCO ili kupata maombi ya umeme kwa njia salama, rahisi na ya haraka, badala ya kutumia njia zisizo halali ambazo huweka maisha na mali zao hatarini.
Shirika hilo limeahidi kuendelea na oparesheni hiyo katika wilaya zote za Mkoa wa Mwanza hadi vitendo vya hujuma na wizi wa umeme vita kapokoma kabisa.