Vijana nchini wametakiwa kujikita katika elimu ya fani zitakazowawezesha kujiajiri, badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini au sekta binafsi, ili kukabiliana na hali halisi ya soko la ajira.
Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) – Kampasi ya Mwanza, Benedicto Rutigadius, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo.
“Tukubaliane na mabadiliko, kwani ni sehemu ya maisha ya sasa. Ajira zimepungua, hivyo ni wakati wa vijana kujiandaa kujiajiri wenyewe,” amesema Rutigadius
Akizungumza katika banda hilo la DIT, mwanafunzi wa chuo hicho, Samwel Mmbaga, ameeleza kuwa elimu aliyopata kwenye uchakataji wa bidhaa za ngozi kama mikanda, viatu na pochi inamwandaa yeye kujitegemea.
“Mafunzo tunayopata ni ya vitendo na yanatupa maarifa ya kutosha kuanzisha ajira zetu wenyewe,” amesema Mmbaga.