Na Mwandishi Wetu – Nanenane, Dodoma
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa mfumo wa JamiiStack umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuunganisha mifumo ya kiserikali na binafsi, hivyo kuchochea maendeleo ya kidijitali nchini Tanzania, hasa kwa wakulima na wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, Afisa TEHAMA wa Wizara hiyo, Kiswigu Mwakisisya, alisema JamiiStack ni mfumo jumuishi unaowezesha mifumo mbalimbali ya kidijitali kusomana, kubadilishana taarifa kwa usalama na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa.
Alieleza kuwa JamiiStack ni mkusanyiko wa teknolojia muhimu za msingi (Digital Public Infrastructure – DPI) ambazo zimeundwa kwa ajili ya kuongeza ubora wa utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali. Teknolojia hizi zimejengwa kwa kuzingatia usalama, faragha na haki za mtumiaji wa mwisho wa huduma hizo.
Kwa mujibu wa Mwakisisa, JamiiStack inahusisha kwanza uwepo wa mazingira wezeshi ya kiteknolojia. Hii inajumuisha kuwepo kwa minara ya mawasiliano, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaounganisha wilaya mbalimbali nchini, na nishati ya umeme inayohitajika kuendesha mifumo ya TEHAMA. Pia, mazingira haya wezeshi yanajumuisha kuwepo kwa miongozo, sera na sheria zinazoratibu matumizi ya TEHAMA kwa usalama na ufanisi.
Aidha, alieleza kuwa sehemu ya pili ya JamiiStack ni miundombinu ya kidijitali ya umma, inayojumuisha mifumo mitatu muhimu: Jamii Namba, Jamii Pay na mfumo wa JamiiStack wenyewe. Kupitia Jamii Namba, kila mwananchi anatambulika rasmi katika mifumo ya kidijitali, kuanzia umri wa miaka 0. Namba hii ya kipekee, kama ile ya NIDA, hutumika katika huduma mbalimbali kwa utambulisho wa haraka na salama. Kwa upande wa Jamii Pay, ni mfumo wa malipo ya kielektroniki unaoratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania kupitia Tanzania Instant Payment System (TIPS), unaowezesha miamala kufanyika kwa haraka na kwa usalama zaidi.
Mwakisisya alifafanua kuwa sehemu ya tatu ya mfumo wa JamiiStack ni ile inayohusu ubadilishanaji wa taarifa kwa usalama baina ya mifumo ya taasisi za serikali na sekta binafsi. Kupitia mfumo wa Jamii X-Change, taasisi zinaweza kushirikiana taarifa kwa viwango sanifu vya kitaifa, bila kuhatarisha faragha ya watumiaji wa huduma, na hata kubadilishana taarifa zinazovuka mipaka ya nchi kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia manufaa ya JamiiStack kwa wakulima, Afisa huyo alisema mfumo huo unasaidia kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuwapatia wakulima taarifa muhimu kuhusu hali ya hewa, tabia ya udongo, na magonjwa ya mazao. Taarifa hizi hupatikana kwa urahisi kupitia simu janja, mitandao au hata redio jumuishi zinazofikia maeneo ya vijijini. Hii inamwezesha mkulima kupanga kilimo kwa ufanisi zaidi, hivyo kuongeza mavuno.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa katika kukuza mazingira ya TEHAMA kwa kujenga miundombinu mikubwa, ikiwemo Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ambalo si tu linaongeza nishati ya umeme kwa matumizi ya viwanda na majumbani, bali pia linatoa mchango muhimu katika maendeleo ya kidijitali nchini.
Kwa ujumla, JamiiStack imeonekana kuwa msingi imara wa mageuzi ya kiuchumi kupitia teknolojia. Mfumo huu unaiweka Tanzania katika ramani ya maendeleo ya kidijitali barani Afrika, kwa kuunganisha nguvu kati ya sekta ya umma na binafsi katika utoaji wa huduma bora, salama na zenye tija kwa wananchi wote, hususan wakulima walioko vijijini.