Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pembejeo, Bw. Itandula Gambalagi, amesema kuwa Mfuko huo umechangia kiasi cha shilingi bilioni 8.5 kwa Benki ya Ushirika (COOP Bank) kwa ajili ya kuwezesha wakulima nchini kupata mikopo nafuu ya pembejeo na mitaji ya kilimo.
Akizungumza leo Agosti 5, 2025, katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Bw. Gambalagi alisema kuwa fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Mfuko na Benki ya Ushirika kupitia Hati ya Makubaliano (MOU) iliyosainiwa Aprili 2025 mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima, leo tunakabidhi mfano wa hundi ya shilingi bilioni 8.5 kwa Benki ya Ushirika. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 5 ni Mkopo wa Jumla (Wholesale Loan) wa miaka mitano wenye riba nafuu ya asilimia 3,” alieleza.
Kwa mujibu wa Bw. Gambalagi, sehemu nyingine ya fedha hiyo itatumika kama dhamana ya mikopo (Credit Guarantee) kwa Benki ya Ushirika ili iweze kukopesha wakulima wadogo ambao hawana dhamana au dhamana zao hazitoshelezi. Vilevile, Mfuko umefungua akaunti maalum ya uendeshaji (Operational Account) katika benki hiyo kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa makubaliano hayo.
Alifafanua kuwa Benki ya Ushirika itakuwa na jukumu la kupokea na kuchakata maombi ya mikopo kwa niaba ya Mfuko wa Pembejeo, na kutoa taarifa za kila mwezi kuhusu mikopo inayotolewa, ikiwa ni pamoja na majina ya wanufaika, kiasi cha mkopo, mkoa, wilaya, matumizi ya mkopo, muda wa mkopo na marejesho.
“Mashirikiano haya yanalenga kuongeza kasi ya utoaji mikopo kwa wakulima wengi zaidi nchini kupitia Benki ya Ushirika yenye matawi manne na mawakala walioko karibu na wakulima,” alisema.
Bw. Gambalagi aliishukuru Benki ya Ushirika kwa ushirikiano uliopo hadi sasa, na kusisitiza kuwa fedha hiyo ya umma inapaswa kutumika kwa ufanisi ili kutoa matokeo chanya katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha kaya.
“Nitumie fursa hii kuhimiza utekelezaji makini wa mikopo hii ili ifikie walengwa kwa ufanisi na kuongeza tija kwa taifa,” alihitimisha.