Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe akizungumza na washiriki wa programu ya KAIZEN katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa program hiyo ambayo inahusisha viwanda vidogo na vikubwa iliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Februari 18, 2020.
Balozi wa Japan Nchini Tanzania, Mhe. Shinichi Goto, akizungumza na
washiriki wa programu ya KAIZEN katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa
programu hiyo ambayo inahusisha viwanda vidogo na vikubwa iliyofanyika katika
Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Februari
18, 2020.
Mkurugenzi wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw.Leo
Lyayuka akitoa neno la shukurani kwa washiriki wa programu ya KAIZEN katika
hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa program hiyo ambayo inahusisha viwanda
vidogo na vikubwa iliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Februari 18, 2020.
Wawakilishi kutoka kiwanda cha Shelly’s Pharmaceutical Tanzania,
wakipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara,
Prof.Riziki Shemdoe, baada ya kutangazwa washindi wa kwanza katika programu
ya KAIZEN kundi la viwanda vikubwa katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi
wa programu hiyo iliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Februari 18, 2020.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe, akiwa
kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara na
KAIZEN mara baada ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa Programu hiyo katika hafla
iliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam leo Februari 18, 2020.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe, akiwa
kwenye picha ya pamoja na washindi wa tuzo za KAIZEN mara baada ya kukabidhi
tuzo hizo katika hafla iliyofanyika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam leo Februari 18, 2020.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.
***************************
NA EMMANUEL MBATILO
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Profesa Riziki Shemdoe, ametaka falsafa ya KAIZEN kutumika katika sekta zote nchini ili kujenga uwezo kwa jamii wa kuzingatia ubora na kuongeza tija ya shughuli za kila siku.
Alisema pia matumizi ya falsafa hiyo yatasaidia urahisi wa utoaji huduma kwa umma katika taasisi za kijamii, hivyo ni vyema ijengewe msingi wa kutekelezwa kuanzia ngazi ya familia.
Hayo ameyasema leo wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo ya washindi wa mashindano ya nne ya KAIZEN kitaifa yanayoratibiwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Amesema falsafa hiyo inahusu matumizi ya mbinu bunifu katika kuongeza ubora na tija ambayo kwa sasa inatekelezwa zaidi viwandani, hivyo ni vyema ingeambukizwa kwa sekta zote ili ilete manufaa.
Ameongeza kuwa kwa upande wa viwanda falsafa ya KAIZEN imekuwa chachu ya kuviwezesha kuhimili ushindani.
“Sababu ya kutaka falsafa hiyo kutumika hadi katika sekta nyingine kama elimu na afya ni kwamba mnyororo wa thamani wa viwanda ni fungamani na sekta nyingine”. Amesema Prof.Shemdoe.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania Shinichi Goto, amesema kupitia falsafa hiyo kuna mwelekeo wa Tanzania kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda.
Amesema pamoja na sababu nyingine zinazofanya Tanzania kuimarika kiuchumi pia falsafa hiyo ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi kwani ndio inayotumika na taifa la Japan hadi kufikia mafanikio iliyonayo sasa.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa serikali kuhakikisha inakuza uelewa wa jamii juu ya falsafa hiyo kuanzia shule za awali.
Naye Mwakilishi wa JICA nchini Tanzania Naofumi Yamamura, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuhakikisha inaleta tija katika uzalishaji viwandani na kuendana na sera za nchi.
Amesema ushiriki wa Viwanda katika mashindano ya taifa ya KAIZEN inaleta chachu kwa viwanda vidogo kuongeza juhudi ili kufikia mafanikio makubwa.