Home Mchanganyiko OFISA ELIMU NYASA AWACHARUKIA WALIMU WAKUU NA MAAFISA ELIMU KATA

OFISA ELIMU NYASA AWACHARUKIA WALIMU WAKUU NA MAAFISA ELIMU KATA

0

Ofisa Elimu msingi Wilaya ya Nyasa Bw. Said Kalima akiongea na Walimu wakuu na Maafisa Elimu kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa jana, Katika ukumbi wa Kasimu Majaliwa ulioko katika shule ya Sekondari Mbamba-bay wilayani hapa.Amewaagiza walimu hao kufundisha kwa bidii na kutomvumilia mwalimu mzembe na kupandisha ufaulu ufikie asilimia mia moja kwa Wilaya ya nyasa,kuanzia mwaka huu 2020 na kuendelea.

……………………………………………………………………………………….

Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Nyasa Said Kalima, amewataka walimu wakuu na Maafisa
Elimu Kata, kuwasimamia walimu ili wafundishe kwa bidii ili kupandisha ufaulu Wilayani hapa.
Maagizo haya aliyatoa jana, wakati akiongea na walimu wakuu wote, na Maafisa Elimu Kata
Wilayani hapa, walipokuwa wakifundishwa kutumia mfumo wa premu, katika Ukumbi wa wa
kisasa wa Kassimu Majaliwa, uliopo katika Shule ya Sekondari Mbamba-bay Wilayani nyasa kwa
lengo la kuwekeana mikakati ya kuhakikisha ufaulu unapanda kwa 100% (asilimia mia moja).
Bwana Kalima alifafanua kuwa, imefika wakati kila mwalimu atambue wajibu na majukumu
yake na kufanya kazi kwa bidii, ili kupandisha ufaulu katika Wilaya ya Nyasa. Walimu wakuu na
Maafisa Elimu Kata ni Wasimamizi wakuu wa kila siku wa kuhakikisha walimu wanajituma, na
kufanya kazi ya kufundisha wanafunzi kwa bidii, kwa kuwa kila mwalimu akisimamiwa vizuri na
akatekeleza majukumu yake, Ufaulu nyasa utapanda na kufikia100% (asilimia mia moja).
Aliongeza kuwa hatasita kuchukua hatua za haraka kwa mwalimu mkuu yeyote atakayeshindwa
kusimamia ufaulu katika Shule yake, kwa kuwa atafanya ukaguzi wa kushtukiza katika shule
zote wilayani hapa, ili kubaini mapungufu, na kuchukua hatua mara moja ikiwa ni pamoja na
kumshusha madaraka mwalimu, mwalimu mkuu au Ofisa Elimu kata na kumchukulia hatua za
kinidhamu ikiwa ni pamoja na hatua zaidi za kiutumishi.
“Nachukukua Fursa hii kuwaagiza ninyi Maafisa Elimu Kata na Walimu wakuu, kuhakikisha kuwa
mnawasimamia walimu wenu, na kuhakikisha wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa. Kwa kuwa
nyie ni viongozi katika maeneo yenu. Mkihakikisha mnatekeleza majukumu yenu katika shule
na Kata zenu Halmashauri hii itakuwa na ufaulu mzuri, na kuhakikisha tunafika asilimia mia
moja. Ukiwa na cheo hakikisha unakitumia vizuri, kwa lengo la kuisaidia jamii. Kama hawa
wanafunzi wakifaulu kwa 100% (asilimia mia moja) unakuwa umefuta ujinga kwa wananchi
wengi na unakuwa umeipa maendeleo jamii. Nitawachukulia hatua mara moja endapo nikipata
taarifa ya mwalimu mtoro, mvivu, au asiyewajibika ipasavyo,”. Alisema Kalima
Aidha aliwaagiza viongozi hao kutoa taarifa za haraka na mapema kukiwa na matukio ya walimu
watoro,wavivu na wasioshirikiana na viongozi hao au kutokutekeleza maagizo kwa wakati naye
atachukua hatua mara moja.

Ofisa Elimu huyo aliwaagiza walimu wakuu na maafisa Elimu kata kuhakikisha wanafanya
mazoezi/majaribio ya siku,wiki,mwezi, na mitihani ya Kata ya ujirani mwema na Wilaya kwa
madarasa ya Mitihani ili kuwaweka sawa wanafunzi ili waweze kujiandaa vema na mitihani.
Aidha, katika hatua nyingine alimpongeza mh Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania John
pombe Magufuli kwa kuhakikisha miundombinu ya Elimu ya Wilaya ya Nyasa inavutia na kuwa
rafiki kwa mazingira ya kujifunzia.Hivyo alitoa siku saba kuhakikisha walimu wakuu wote
waliopokea fedha za ujenzi wa miundombinu inakamilika.
“Mh Rais ametupendelea sana wana Nyasa,ametupa fedha za kujengea miundombinu ya Elimu
na anatoa Elimu bila malipo, hata ukipita kwenye shule zetu za msingi madarasa yanapendeza
na vyoo pia vinapendeza, kwa hiyo kazi iliyobaki ni kumuenzi kwa kuhakikisha ufaulu unakuwa
kwa 100% (asilimia mia moja) kwa Wilaya ya Nyasa kwa mwaka 2020 na kuendelea” Alisema
Kalima.