Na John Bukuku – Dodoma
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewasilisha teknolojia mpya ya kisasa ya umwagiliaji kwa kutumia mfumo wa njia ya mvua (CENTER PIVOT) Center Pivot katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za mageuzi ya sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia bunifu.
Akizungumza leo Agosti 2, 2025 katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali, Maria Itembe, amesema teknolojia hiyo ni mpya kwa matumizi ya taasisi hiyo, ambapo imekuwa ikitumika kwa mataifa mbalimbali lengo likiwa ni kuleta mageuzi katika kilimo cha Umwagiliaji.
“Mwaka huu tumekuja na vitu vingi vipya tunacho kijiji cha mitambo ambapo kuna mitambo mbalimbali ikiwemo mfumo wa umwagiliaji wa mvua, magari yenye mitambo za uchimbaji visima, mabwawa na mengine mengi ambayo hayakuwepo maonyesho yaliyopita.
“Nyuma yangu kuna mitambo mikubwa ya kumwagilia – hii ni Center Pivot, teknolojia mpya tunayoweka kwa sasa katika maeneo ya umwagiliaji,” amesema Itembe.
Ameongeza kuwa teknolojia hiyo tayari imeanza kufungwa katika mashamba ya miradi ya umwagiliaji mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo, kama sehemu ya kuongeza tija na uzalishaji.
“Tumejipanga ipasavyo na tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt Isidori Mpango alipofungua maonyesho ya mwaka huu ambapo, amehimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye kilimo. Tunaamini kupitia mitambo iliyopo, wakulima wataweza kujifunza mengi na kufikiwa na huduma za Umwagiliaji katika maeneo yao kwani fursa hizi zipo kila mahali mikoani kote tumewafikia hivyo ni wakati sasa Watanzania kuchangamkia fursa za Kilimo cha Umwagiliaji kwa kulima mwaka mzima bila kutegemea mvua,” amefafanua.
Kwa mujibu wa Itembe, amesema matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza ufanisi wa kilimo na kuwasaidia wakulima kuvuna mara kwa mara kwa mwaka, hivyo kuongeza kipato chao na kuchochea uchumi wa taifa.
Aidha, amebainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za serikali za uwekezaji sekta ya kilimo kwa kuongeza maeneo ya umwagiliaji kutoka hekta 500,000 hadi 980,000, huku lengo la serikali likiwa ni kufikia hekta 1,200,000 za Umwagiliaji nchini.
“Maendeleo haya yametokana na ongezeko kubwa la bajeti ya Tume ya Umwagiliaji kutoka Shilingi bilioni 46 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 403 mwaka huu wa fedha,”amesema.
Amesisitiza kuwa licha ya gharama kubwa za ununuzi wa mitambo ya kisasa, hatua hiyo imewezekana kutokana na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti na kuwekeza kwa dhati katika sekta ya umwagiliaji.