DENIS MLOWE, MAFINGA
MTIA nia katika nafasi ya Ubunge Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Luqman Merhab amejirahishia nafasi ya kuchaguliwa na wajumbe kutokana ahadi zake katika kura za maoni kuwateka wapiga kura licha ya kanuni zinakataza wajumbe kushangalia hali ambayo imekuwa tofauti kwa upande wake.
Jimbo la Mufindi Kaskazini ambalo mbunge wake aliyepita ni Exaud Kigahe linagombewa na wagombea watano katika kutia nia ambao kila mmoja amesimama mbele ya wajumbe wa Chama cha Mapinduzi kutaka kuteuliwa nafasi ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wagombea wametoa ahadi zao katika kata za Mdaburo, Ifwagi na Ihanu ambapo Merhab akionekana kuwakosha zaidi wajumbe huku akitumia msemo ukiwa na panya ndani ya nyumba usiangalie rangi ya paka angalia paka anayeweza kwenda kukamata panya.
Merhab akizungumzia kuhusu miundo mbinu ya barabara aliomba wajumbe wampe kura awe mwakilishi ili aweze kushirikiana na serikali kupitia kampuni yake ya ukandarasi kuhakikisha zinapitika kipindi cha Masika.
Alisema kuwa ahadi yake ya barabara haitegemei makadirio ya kisiasa pekee bali inatokana na uzoefu wa kitaaluma na uwezo wa moja kwa moja wa kutekeleza.
Luqman Merhab si mwanasiasa tu yeye ni mkandarasi aliyebobea katika sekta ya ujenzi, mwenye kampuni inayofanya kazi halisi ya kutekeleza miradi ya miundombinu ikiwemo barabara.
Alisema kuwa miaka kadhaa amehusika moja kwa moja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara akifahamu kwa kina kila hatua ya mchakato kuanzia usanifu, bajeti, hadi ujenzi wa mwisho.
Akizungumzia suala la ajira kwa vijana alisema kuwa anafahamu ni changamoto hiyo hivyo wampe nafasi ili avutie wawekezaji waweze kufungua viwanda kila kata ya Mufindi Kaskazini.
Aliongeza kuwa wananchi wa Mufindi Kaskazini wana sababu ya kuamini kwamba kwa mara ya kwanza, wanaye mgombea ambaye anapozungumzia miundombinu ya barabara, anazungumzia jambo analolifanya kila siku na ana nguvu kama kijana kuweza kuwatumikia.
“Changamoto za Mufindi Kaskazini nazijua hivyo mnitume niende nikatatue changamoto za barabar za mdaburo na jimbo zima kwa ujumla na kuongeza kuwa suala la umeme nalo atalitendea haki kwa kutoa nguzo bure kabisa ili wananchi wapate umeme Mimi sio mtu wa maneno ni vitendo ” alisema
Akizungumzia kuhusu kiwanda kilichoko kata ya Ifwagi cha chai Itona aliomba wajumbe wampe kura akiwa mbunge ahakikishe kinafanya kazi na kuleta ajira kwa vijana.