Na Silivia Amandius
Bukoba, Kagera
Mbunge wa Bukoba Mjini, Adv. Stephen Byabato, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao, huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuimarisha maendeleo, licha ya maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM kutomteua kuendelea kugombea nafasi hiyo.
Byabato ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini na mkoa wa Kagera kwa ujumla kupitia kituo kimojawapo cha redio mkoani Kagera, ambapo alisisitiza mshikamano na mshirikiano kati yake na wananchi kuwa ndio msingi wa kuendeleza maendeleo. Aidha, alibainisha kuwa hana kinyongo na maamuzi ya chama chake na akawataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa amani katika kipindi cha uchaguzi.
Mbunge huyo pia alieleza kuwa gari la jimbo litaendelea kutoa huduma kama kawaida, huku akifafanua kuwa utaratibu mdogo wa usafiri pekee ndio utakaobadilika ili kuendeleza msaada wa kijamii kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo. Alisisitiza kuwa dhamira yake ni kuona kila mkazi wa Bukoba anafaidika na rasilimali za jimbo hilo.
Katika kipindi cha uongozi wake, Byabato ameacha alama kubwa kupitia ujenzi wa barabara nne zenye urefu wa kilomita 10, daraja jipya linaloendelea kujengwa na kufikia asilimia 44, na kuboreshwa kwa kingo za Mto Kanoni kwa gharama ya TZS bilioni 7.3 ili kudhibiti mafuriko. Aidha, ujenzi wa barabara za mitaa na stendi mpya kwa gharama ya TZS bilioni 10.75, pamoja na soko kuu la kisasa lenye thamani ya TZS bilioni 42.2, ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuongeza fursa za biashara na kipato kwa wakazi wa Bukoba.
Kupitia miradi hiyo, taa za barabarani zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya manispaa, hatua iliyoongeza usalama na kuboresha mandhari ya mji. Wananchi sasa wanaona mabadiliko halisi katika maisha yao ya kila siku, kutokana na uwekezaji wa miradi hii ya miundombinu na kijamii.
Byabato amehitimisha kwa kuwataka wananchi waendelee kushiriki mchakato wa uchaguzi kwa amani, kulinda na kuimarisha miradi iliyopo, akisisitiza kuwa huduma na maendeleo jimboni Bukoba hayatakoma kwa sababu ya mabadiliko ya kisiasa, kwani uongozi wa vitendo huishi kwa matokeo, si kwa nafasi pekee.