NA DENIS MLOWE, IRINGA
TIMU ya Soka ya Kising’a fc imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano ya kombe la Vunjabei baada ya kuibabua timu ya soka ya BBC fc kwa magoli 3- 0 katika mchezo wa nusu fainali ya pili.
Katika mtanange huo uliopigwa katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege hadi kipindi cha kwanza kinaisha BBC walishakubali kipigo cha magoli 2.
Katika mchezo huo magoli ya Kising’a yalifungwa na Isack Sakula katika dakika ya 17 wakati goli la pili lilifungwa na Nuhu Msola katika dakika ya 31.
Kipindi cha Pili kilianza kwa BBC kutaka kurudisha magoli hayo mawili huku Kising’a fc nao wakifikiria namna gani ya kuongeza magoli zaidi.
Katika dk ya 73 ya mchezo timu ya Kising’a Fc ilifanikiwa kupata bao lilofungwa na Gift Sanga hali iliyodidimiza kabisa matumaini ya BBC fc kutinga hatua ya Fainali.
Kwa matokeo hayo Kising’a f watakwenda kuumana vikali na timu ya Mgela Fc iliyofanikiwa kutinga hatua ya fainali tangu wiki iliyopita.
Michuano hiyo inadhaminiwa na kampuni ya Vunja Bei chini ya Fred Ngajilo aka Fred Vunjabei itatoa zawadi kwa mshindi wa kwanza (milioni 10), mshindi wa pili (milioni 3), na mshindi wa tatu (milioni 2). Pia kutakuwa na zawadi za mchezaji bora, mfungaji bora, kipa bora, mashabiki bora, na waandishi wa habari.