Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, akizungumza katika Kongamano la Kitaaluma la Kujadili Ubia wa Sekta Binafsi na Umma katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililofanyika Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza, leo.
Dkt.Jasinta Msamula, wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, akiwaslisha mada ya nafas ya PPP kukuza Uwekezaji na Ufanisi katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa ,leo, katika kongamano la Dira ya 2050. (Picha zote na Baltazar Mashak)
………….
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema kuwa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hususan baada ya maboresho ya sheria mbalimbali yaliyowezesha ushirikiano huo.
Akizungumza katika Kongamano la Kitaaluma la Kujadili Ubia wa Sekta Binafsi na Umma katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza, leo, Kafulila ameeleza kuwa dira hiyo inalenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
“Hili ni lengo kubwa, lakini linawezekana iwapo kila sekta itaweka vipaumbele vyake kulingana na malengo ya dira. Ni lazima tuwekeze katika maeneo muhimu kama kilimo, afya, elimu na maji, ambavyo vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini,” amesema Kafulila.
Amebainisha kuwa ili kutimiza malengo hayo, ni lazima kutafuta mbinu mpya za upatikanaji wa rasilimali fedha, na ndiyo maana ubia wa sekta binafsi unahamasishwa huku akitaja sababu tatu kuu za kushirikiana na sekta binafsi kuwa ni: kupatikana kwa mtaji, teknolojia ya kisasa, na ufanisi wa uendeshaji wa miradi.
“Hadi sasa, ni nchi 19 tu duniani zilizofikia uchumi wa trilioni moja. Barani Afrika, ni Afrika Kusini pekee iliyofikia kiwango hicho. Ili tufikie huko, lazima tujenge uchumi unaokua kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka, jambo linalohitaji mabadiliko ya fikra, sera na sheria,” amesisitiza.
Aidha, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa PPPC amesema kuwa Dira ya 2050 inalenga kuongeza pato la wastani kwa kila Mtanzania hadi kufikia dola 7,000 kwa mwaka, akionya kuwa ongezeko kubwa la idadi ya watu linaweza kuathiri ustawi wa taifa iwapo halitazingatiwa.
“Wastani wa ukuaji wa watu duniani ni asilimia 1, Afrika asilimia 2, lakini Tanzania ni zaidi ya asilimia 3. Ongezeko hili linaifanya serikali kubeba mzigo mkubwa wa utoaji huduma za kijamii, hasa kwa nchi inayojijenga kiuchumi kama yetu,” amefafanua.
Amesisitiza kuwa jamii haina budi kubadili mtazamo na kuwajibika katika kupanga familia kwa kuzingatia uwezo wa kuwalea watoto, ili kupunguza utegemezi kwa serikali.
Kafulila ameongeza kuwa ubia si jambo jipya, bali hata mataifa mengine yaliyoendelea yanatekeleza miradi mingi kwa kushirikiana na sekta binafsi,hivyo Tanzania nayo imechukua hatua kwa kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuruhusu na kuimarisha ushirikiano huo.
“Taasisi za umma ambazo zimeingia katika ubia zimeshuhudia mafanikio ya kiuchumi. Ubia unarahisisha upatikanaji wa mitaji na kuifanya serikali kutekeleza miradi nje ya ukomo wa bajeti yake ya kawaida,” amesema.
Hata hivyo, Kafulila alikiri baadhi ya sekta zenye umuhimu mkubwa hazivutii wawekezaji binafsi kwa kutokutoa faida ya moja kwa moja kibiashara,lakini ipo miradi inayolipa kiuchumi si kibiashara,miradi hiyo ni muhimu na haina budi kutekelezwa kwa kushirikiana baina ya serikali na sekta binafsi ili kufanikisha Dira ya 2050.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Profesa. Balozi Adelardus Kilangi, ametahadharisha kuhusu changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya ubia akisema kuna tatizo la taasisi za umma kutokuwa na mwelekeo wa pamoja,ipo haja ya kufanya utafiti kubaini vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji mzuri wa miradi ya PPP.
“Tunahitaji kufanya uchambuzi wa kina wa sheria za uwekezaji na mikataba, hasa katika mazingira ya kimataifa. Changamoto nyingi zinazojitokeza si kwa sababu ya udhaifu wa sheria zetu, bali kutokana na sheria za kimataifa tunazotakiwa kuzifuata,” amesema Prof. Kilangi , huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia mlingano kati ya siasa, uchumi na sheria katika kusimamia uzalishaji na mgawanyo wa utajiri wa taifa.
Hivyo, kwa maoni na ushauri kuhusu ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa, wananchi wanahimizwa kufuatilia mijadala ya kitaaluma kama huo ili kuchangia mustakabali wa taifa letu.