Na Sophia Kingimali.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Abdallah Mitawi amesema Serikali imeridhishwa na mchango wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) katika kukuza uchumi wa buluu nchini, huku ikiahidi kuimarisha ushirikiano na taasisi hiyo ili kufanikisha utekelezaji wa sera mpya ya uchumi wa buluu ya mwaka 2024.
Akizungumza mara baada ya ziara chuoni hapo, leo Julai 25,2025, amesema kuwa ziara hiyo ilikuwa na lengo la kufahamiana na kujifunza shughuli zinazofanywa na DMI, pamoja na kuangalia maeneo ya ushirikiano katika kutekeleza mkakati wa uchumi wa buluu.
“Tumekuja hapa kujifunza na kuona namna bora ya kushirikiana, hususan katika eneo la utafiti ambalo ni nyeti sana kwa maendeleo ya uchumi wa buluu. Bila utafiti wa kina, ni vigumu kutekeleza kwa ufanisi mkakati huu,” amesema Mitawi.
Amebainisha kuwa DMI ni miongoni mwa taasisi muhimu kwenye sekta ya uchumi wa buluu na imekuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti tangu kuanzishwa kwake mwaka 1978, huku ikiendelea kutambulika kimataifa.
Amesema kuwa tangu mwaka 2021, DMI imekuwa ikiandaa makongamano ya uchumi wa buluu yanayoshirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika, jambo linalothibitisha mchango mkubwa wa chuo hicho katika sekta hiyo.
“Mwaka huu kongamano lilifanyika Gambia, na linatarajiwa kufanyika tena kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Hii inaonesha namna gani DMI limejikita kikamilifu katika kukuza sekta hii,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Prof. Tumaini Gurumo, amesema kuwa ujio wa uongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ni ishara ya kutambuliwa kwa juhudi za DMI katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu.
“Sisi kama chuo tumekuwa sehemu ya mchakato mzima wa kuundwa kwa sera na sasa tumepewa jukumu maalum la kuratibu tafiti, jambo ambalo tunalichukulia kwa uzito mkubwa. Tuko tayari kuendelea kufanya ubunifu utakaosaidia taifa kunufaika na rasilimali za baharini,” amrsema Prof. Gurumo.
Aidha, Prof. Gurumo ameongeza kuwa DMI imekuwa ikizalisha wataalamu wengi wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi kwenye sekta mbalimbali za uchumi wa buluu kama uchukuzi, utalii na madini, huku programu zake za mafunzo zikiendana na mahitaji ya soko.
Katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni, uchumi wa buluu umewekwa miongoni mwa maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya kuongeza pato la taifa na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.