Na John Bukuku, Dar es Salaam
Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd kwa kushirikiana na TotalEnergies Foundation na NafasiArt Space imezindua rasmi toleo la mwaka 2025 la mradi wa VIA Creative, mradi unaolenga kukuza elimu ya usalama barabarani kwa kutumia mbinu za kisanaa kama muziki, maigizo na sanaa za maonyesho, hususan kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Julai 25, 2025 katika Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, ambapo Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Saadati Mohamed – aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya – amepongeza TotalEnergies kwa kujitoa katika kuhakikisha usalama wa vijana barabarani unaimarika kupitia mbinu shirikishi na za ubunifu.
“Usalama barabarani hauishii tu kwenye barabara nzuri, bali unahitaji uelewa, nidhamu, na ushirikiano wa jamii nzima. VIA Creative ni mradi wa kipekee unaotumia vipaji vya sanaa kufikisha elimu hii muhimu kwa vijana wetu,” alisema Saadati.
Amesisitiza kuwa kundi la vijana wa sekondari ni miongoni mwa watumiaji wakuu wa miundombinu ya barabara—ikiwa ni kwa kutembea kwa miguu, kutumia baiskeli au bodaboda—ambavyo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya ajali barabarani.
“Kupitia VIA Creative, tunashuhudia mshikamano wa sekta binafsi na serikali katika juhudi za kuzuia ajali na kuimarisha usalama wa watoto wetu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa TotalEnergies Tanzania, Bi. Getrude Mpangile, alieleza kuwa kati ya mwaka 2022 hadi 2024, VIA Creative iliwafikia wanafunzi zaidi ya 22,000 kutoka shule za msingi 60 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
“Mwaka huu tumeamua kupanua wigo kwa kulenga wanafunzi wa sekondari, tukianzia na shule ya Sekondari Ndalala mkoani Dodoma,” alisema Getrude.
Ameeleza kuwa wanafunzi watashiriki kwenye shindano la kitaifa litakalowawezesha kuwasilisha kwa ubunifu maarifa na ujuzi walioupata kuhusu usalama barabarani. Shule itakayoshinda kitaifa itapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda, hatua inayolenga kuimarisha mshikamano wa Afrika na kuendeleza maadili ya usalama barabarani.
Aidha, Getrude amesema kuwa washindi wa kitaifa pia watapewa nafasi ya kutekeleza mapendekezo yao ya kuboresha mazingira ya usalama katika shule zao. Mfano halisi ni shule ya msingi ya Makuburi iliyoibuka mshindi mwaka 2024, ambapo pendekezo lao la kujengewa ukuta wa shule liliweza kutekelezwa kwa mafanikio, na hivyo kuwaepusha wanafunzi na hatari za magari na bodaboda zilizokuwa zikipita karibu na uwanja wa shule.
“Hii ni njia ya kuwajengea wanafunzi si tu maarifa bali pia ujasiri wa kutoa suluhisho katika jamii zao,” alihitimisha.
Mradi wa VIA Creative unaendelea kuwa mfano wa ubunifu katika kushirikisha vijana, walimu na jamii nzima katika harakati za kupunguza ajali barabarani, huku ukitoa jukwaa la kukuza vipaji vya kisanaa kwa ajili ya maendeleo ya kijamii.