Na Farida Mangube, Morogoro
Wananchi wa Kijiji cha Sesenga, Wilaya ya Morogoro, wanatarajia kunufaika moja kwa moja na ajira, uboreshaji wa miundombinu na uchumi wa mtu mmoja mmoja kufuatia kuanzishwa kwa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini adimu na muhimu (Rare Earth Elements) katika eneo la Mlima Wigu.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), utafungua fursa nyingi kwa vijana, wanawake na wazazi wa eneo hilo kupitia ajira na huduma zinazotokana na shughuli za uchimbaji.
“Kutakuwa na mzunguko mkubwa wa fedha, mahitaji yatakuwa makubwa, hivyo wananchi watanufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira kwa kina mama na vijana,” alisema Waziri Mavunde wakati wa hafla ya kukabidhi leseni ya uchimbaji kwa STAMICO iliyofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Sesenga.
Serikali imetenga eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 15.4 (sawa na hekari 3,557) kwa ajili ya mradi huo, ambao unatarajiwa pia kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia ushuru wa huduma.
Waziri Mavunde alibainisha kuwa mradi huo ni matokeo ya maboresho ya sheria ya madini, ambapo wamiliki wa leseni sasa wanatakiwa kurudisha kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo. Aliziagiza serikali za vijiji kuandaa miradi wanayotaka ifadhiliwe kupitia mapato ya mradi huo.
Wananchi wa Sesenga walipongeza hatua hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kushirikishwa moja kwa moja katika ajira na mafunzo yatakayowezesha wao wenyewe kujinufaisha na madini hayo.
“Isiwe kawaida kwa miradi kuwa ya wageni. Tunataka na sisi wenyeji tuwe sehemu ya mradi huu.” Alisema Mwenyekiti wa kijiji hicho, Vicent Andrew.
Mwenyekiti wa wachimbaji madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA), Dk. Omary Mzeru, aliitaka Serikali kuwawezesha wachimbaji wa ndani kwa vifaa na masoko ili waweze kuchimba kitaalamu na kukuza pato la taifa.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Beatrice Njawa, alisema sekta ya madini ni ya tatu kwa uzalishaji kwa mkoa huo, na kwamba mradi wa Wigu utazalisha ajira nyingi na kusaidia wachimbaji wadogo kukua.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse, alisema shirika lake limejipanga kuanza kazi kwa kushirikiana na wananchi, kuanzia kwa walinzi wa eneo hilo waliokuwepo tangu mwanzo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, aliahidi kutoa ulinzi wa kutosha kwa wawekezaji na kuwataka wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi kama njia ya kuthamini juhudi za maendeleo ya Serikali.