Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Thabit Mahamod Kombo, akifungua Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo Julai 24, 2025.
Katibu Mkuu wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi akizungumza katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo Julai 24, 2025,
…………..
Na John Bukuku – JNICC, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Thabit Mahamod Kombo, leo Julai 24, 2025, amefungua rasmi Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi Kombo amesema kuwa ajenda ya mwaka huu ni pana kwa kiasi kikubwa, ikionyesha wigo mpana wa shughuli zilizotekelezwa na Chombo husika cha SADC katika kipindi cha mwaka 2024–2025. Alibainisha kuwa mkutano huo unaashiria kilele cha juhudi zilizofanywa na kamati kuu mbalimbali ndani ya SADC kama vile Kamati ya Masuala ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya nchi, Kamati ya Ulinzi na Usalama kati ya nchi, Kamati Ndogo ya Usalama wa Umma, na Kamati Ndogo ya Usalama wa Ndani ya nchi.
“Waheshimiwa Mawaziri, tunapofakari maendeleo ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri la 27, ni faraja kubaini kuwa asilimia 70 ya maamuzi hayo yametekelezwa na Sekretarieti pamoja na nchi wanachama. Hili linadhihirisha dhamira yetu ya pamoja katika kujenga amani na utulivu wa kudumu katika kanda yetu,” alisema Balozi Kombo.
Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa kipindi hiki kimethibitisha dhamira ya SADC katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia, ambapo nchi wanachama nne—Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia—zimefanikiwa kufanya chaguzi kuu kwa utulivu mkubwa. Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa SADC (SEOM) ulitumwa katika nchi hizo na kushuhudia mchakato mzima wa uchaguzi ukifanyika kwa utaratibu na amani.
Katika maelezo yake, Balozi Kombo alitumia nafasi hiyo kutangaza rasmi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025, na kuiomba SADC kutuma ujumbe wa uangalizi kushuhudia mchakato huo. Aliongeza kuwa nchi za Malawi na Ushelisheli pia zimepanga kufanya chaguzi mwezi Septemba 2025, akiwatakia mafanikio mema.
“Wajumbe Wapendwa, kanda yetu inaendelea kufanya kazi ya kupongezwa katika kuhimiza na kuimarisha amani na usalama. Mfumo wa Tahadhari za Mapema na Baraza la Wazee vinaendelea kutoa mchango mkubwa, na mwaka huu tumezindua Mtandao wa Wanawake Wanaoshiriki katika Usuluhishi ambao ni jukwaa muhimu katika kujumuisha masuala ya wanawake na watoto katika mchakato wa amani,” aliongeza.
Akizungumzia hatua ya hivi karibuni ya viongozi wa SADC kusitisha Ujumbe wa SADC nchini DRC, Waziri Kombo alifafanua kuwa hatua hiyo haikuwa kwa hofu bali ni nafasi ya kuipa diplomasia nafasi kupitia kuunganisha michakato ya amani ya Nairobi na Luanda chini ya mpango wa pamoja wa EAC-SADC. Alisema hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi wa DRC na kanda kwa ujumla.
Aidha, aliipongeza SADC kwa hatua mbalimbali katika sekta ya ulinzi, ambapo zoezi la kuondoa kikamilifu SAMIDRC limefanikiwa na mchakato wa kuanzisha Ghala la Kanda la Kimkakati unaendelea vizuri. Katika eneo la usalama wa umma, nchi wanachama zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka na kuenea kwa silaha ndogo ndogo haramu.
Katika mapambano dhidi ya rushwa, Waziri Kombo alisema nchi wanachama zimeendelea kutekeleza Mpango wa Kimkakati wa Kupambana na Rushwa wa SADC na kuandaa Kielelezo cha Jitihada za Kikanda, ambacho tayari kimefanyiwa majaribio nchini Mauritius na Tanzania. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha Kituo cha Kukabiliana na Ugaidi cha Kanda (RCTC) kilichopo Dar es Salaam ili kiweze kuongoza juhudi za kikanda katika kupambana na ugaidi.
Kwa kumalizia, Balozi Kombo alisisitiza kuwa mshikamano wa SADC ni sehemu ya historia na utambulisho wa kanda hii, na kwamba mafanikio ya sasa yanapaswa kuongozwa na misingi hiyo. Alihimiza nchi wanachama kuendelea kushikamana katika utekelezaji wa mkataba wa SADC na Dira ya Maendeleo ya 2050 ili kuiweka kanda katika nafasi bora zaidi ya maendeleo, mshikamano na amani endelevu.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya kisiasa, kiusalama na maendeleo ya jumuiya hiyo kwa lengo la kuimarisha mshikamano na mafanikio ya pamoja.
Awali Katibu Mkuu wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi akizungumza katika mkutano huo, amesema Kiini cha dira ya SADC kuhusu kuunganisha na kuendeleza kanda hii ni ahadi yetu ya kudumu ya kuhakikisha amani, utulivu na utawala bora. Kwa kuendana na dira hii, mkutano huu utapitia maendeleo ya utekelezaji wa mikakati muhimu ya amani na usalama katika kanda, huku tukithibitisha kwa pamoja dhamira yetu ya kuimarisha usalama wa kikanda, kudumisha taasisi za kidemokrasia, na kuongeza uimara wa jumuiya yetu.
Katika kukabiliana na mgogoro ulioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), SADC ilituma kikosi cha SAMIDRC mwezi Desemba 2023 ili kusaidia juhudi za Serikali ya DRC katika kurejesha amani na usalama. Ili kuimarisha ujumbe huo, SADC ilishirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia Mkutano wa Pamoja wa Viongozi uliofanyika tarehe 8 Februari 2025 hapa jijini Dar es Salaam, hatua iliyothibitisha mshikamano wa kikanda na utekelezaji wa pamoja.
Mikutano ya viongozi iliyofuata mnamo Februari na Machi 2025 iliidhinisha kuunganishwa kwa Michakato ya Amani ya Luanda na Nairobi, pamoja na kuteuliwa kwa Jopo la Wasaidizi wa Usuluhishi kuongoza mpango huo wa pamoja wa amani. Kufuatia maendeleo yaliyopatikana uwanjani, Mkutano Maalum wa Viongozi wa SADC uliofanyika tarehe 13 Machi 2025 uliidhinisha kuondolewa kwa awamu kwa kikosi cha SAMIDRC, zoezi ambalo lilianza rasmi tarehe 29 Aprili 2025 na sasa liko katika hatua za mwisho.
“Tunazishukuru nchi zilizochangia wanajeshi na nchi mwenyeji kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri, na hivyo kuhakikisha ujumbe huu umetimiza malengo yake. Pia tunatoa shukrani kwa Nchi Wanachama zote zilizotoa msaada wa kifedha wa mara kwa mara kwa ujumbe huu,” amesema Bw. Magosi.
Licha ya kukamilika kwa ujumbe huu wa kijeshi, SADC itaendelea kusimama imara pamoja na wananchi wa DRC. Kupitia ushirikiano endelevu wa kikanda na diplomasia, tunaendelea kuamini kwa pamoja kwamba DRC — taifa lenye matumaini makubwa — linaweza kufikia amani ya kudumu, maendeleo jumuishi na heshima ya mwanadamu kurejeshwa, hasa kwa makundi yaliyo hatarini zaidi.
Aidha, kufungwa kwa Ujumbe wa SADC nchini Msumbiji (SAMIM) tarehe 15 Julai 2024 ni hatua muhimu katika juhudi zetu za kurejesha amani katika Mkoa wa Cabo Delgado, mbele ya tishio la ugaidi na misimamo mikali ya kikatili. Hatua hii ni ushahidi wa dhamira ya kanda yetu ya kukabiliana na changamoto ngumu za kiusalama kwa misingi ya maadili, mshikamano, na ushirikiano wa kweli.