Na John Bukuku – JNICC, Dar es Salaam
Katika jitihada za kuendeleza amani na utulivu wa kikanda, viongozi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana leo katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, kujadili changamoto za kiusalama hususan zinazolikumba eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akifungua rasmi mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel W. Shelukindo, amesema kuwa ni jambo la kutia moyo kuona kuwa katika mwaka huu wa tathmini, eneo la SADC limeendelea kuwa na utulivu wa wastani, isipokuwa changamoto za kiusalama zinazondelea katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Balozi Dkt. Shelukindo alibainisha kuwa mzozo huo na hali yake tata vinaendelea kuleta pengo kubwa la kiusalama, hivyo kuhitaji juhudi za pamoja za kikanda na za bara la Afrika kwa ujumla ili kukabiliana na hali hiyo. Alieleza kuwa SADC imekuwa ikitekeleza wajibu wake kupitia kikosi cha SAMIDRC kilichopelekwa nchini DRC tangu mwaka 2023, ambacho kimeisaidia kwa kiasi kikubwa Serikali ya DRC katika juhudi za kurejesha amani.
Hata hivyo, alieleza kuwa kuongezeka kwa mashambulizi ya silaha na kuondoka kwa kikosi hicho kumeibua haja ya kubadili mkakati kutoka wa kijeshi na kuelekea kwenye njia za kisiasa na kidiplomasia.
Akizungumzia juhudi za kuoanisha mikakati ya kuleta amani, Balozi Dkt. Shelukindo alisema kuwa kufanyika kwa Kikao cha Kwanza cha Pamoja cha Viongozi wa EAC na SADC mwezi Februari 2025 jijini Dar es Salaam ni hatua muhimu ya kuunganisha mchakato wa amani wa Luanda na Nairobi, kwa lengo la kuongeza mshikamano na uratibu wa juhudi za kuhakikisha mzozo wa Mashariki mwa DRC unamalizika kwa maelewano ya kudumu.
Alisema kuwa ingawa juhudi hizo za kikanda zinaendelea, ni muhimu pia kutambua na kuunga mkono jitihada za amani zinazoendeshwa na Marekani na Qatar. Msisitizo mkubwa, alisema, unabaki kuwa ni kuhakikisha watu wa Mashariki mwa DRC wanapata amani ya kudumu na utulivu ili waweze kushiriki kikamilifu katika ajenda ya ujumuishaji wa kikanda.
Kwa upande wa maafisa waandamizi wa usalama, aliwasihi kuimarisha uratibu katika ngazi zote—kikanda, bara na kimataifa—ili kuhakikisha juhudi zinafanikiwa kwa ufanisi, kwa gharama nafuu, na kwa njia ya kimkakati. Aidha, alipendekeza kufanyika kwa mikutano ya tathmini (After-Action Meetings) kwa ajili ya SAMIDRC na SAMIM ili kujifunza kutokana na uzoefu uliopatikana na kuandaa kwa ufanisi operesheni zijazo.
Mkutano huo pia uliangazia vitisho vya kiusalama kama vile uhalifu wa kimataifa unaoratibiwa, uhalifu wa mtandaoni, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya—ambavyo Balozi Dkt. Shelukindo alivitaja kuwa ni vikwazo vikubwa kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya SADC 2050.
Akihitimisha hotuba yake, Balozi Dkt. Shelukindo alisema ana matumaini kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya wazi juu ya hali ya usalama wa kikanda kwa mujibu wa nyaraka za kisheria zilizopo. Alitumia fursa hiyo kuwatakia wajumbe wote majadiliano yenye mafanikio na kutangaza rasmi kuwa mkutano huo umefunguliwa.