Na Mwandisi wetu, Hanang
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 Ismail Ussi amewapongeza wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoani Manyara, kwa namna wanavyotekeleza vyema wajibu wao katika usimamizi na ujenzi wa miundombinu.
Ussi ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa daraja lililopo mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang’ katika barabara ya Babati-Gehandu.
Amesema kazi nzuri ya TANROADS imefanikisha ujenzi wa daraja hilo kufuatia maporomoko ya matope kutoka mlima Hanang’ yaliyotokea Desemba 2023 ambapo daraja lililokuwepo lilizidiwa na maporomoko ya matope na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo.
“Tunawapongeza TANROADS Manyara kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ambapo mwisho wa siku wanaonufaika ni wananchi wanaoitumia barabara hii,” amesema Ussi.
Meneja wa TANROADS Mkoani Manyara, mhandisi Dutu Masele ameeleza kwamba mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 18 mwaka 2025 na ujenzi umefikia asilimia 75.
Mhandisi Masele amesema gharama zilizotumika katika ujenzi wa daraja hilo ni shilingi 1,876,054,797,45 ambazo ni fedha kutoka Serikali kuu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa kwa wasafiri wa magari ya abiria mizigo na watembea kwa miguu na kuunganisha wilaya ya Hanang’ na mikoa ya jirani.
Amesema mradi wa daraja hilo unaotekelezwa na mkandarasi ROCKTRONIC LTD chini ya usimamizi wa wakala wa barabara nchini TANROADS, ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa wananchi wa maeneo husika.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mradi huu,” amesema mhandisi Masele.
Kwa upande wake mkazi wa Katesh Sharifa Abdala ameeleza furaha yake ya kuona mwenge wa uhuru ulivyokagua daraja hilo ambalo likikamilika litanufaisha watu wengi hasa wasafiri.