Dar es Salaam. Ifikapo mwaka 2050, Tanzania inajiona kuwa na Mashirika ya umma ya kibiashara yanayoendeshwa kwa uwazi na ushindani, yanayojitegemea na yenye kuleta faida, na yanayovutia uwekezaji huku yakishirikiana kikamilifu na sekta binafsi ili kukuza uchumi.
Dhamira hii imeainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Mhe. Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan, Alhamis, Julai 17, 2025 jijini Dodoma katika tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi akiwemo Bw. Nehemiah Mchechu, ambaye ni Msajili wa Hazina.
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) ndio imepewa jukumu la kuhakikisha ndoto hiyo ya kuyajengea mashirika ya umma ya kibiashara nguvu ya kuwa shindani inafikiwa, kwakuwa ndio msimamizi wa uwekezaji wa mashirika hayo.
OMH inasimamia jumla ya Taasisi, Mashirika ya umma na wakala wa serikali 252, ambapo kati ya hizo, 217 zinatoa huduma na 35 zinafanya biashara.
“Mashirika haya yamekuwa yakipata ruzuku kutoka Serikalini, jambo linaloondoa mazingira ya ushindani kati yao na kampuni binafsi. Hali hii imesababisha kupungua kwa ufanisi wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya taifa,” inasema sehemu ya Dira ya Taifa 2050.
Dira inaenda mbali kwa kuonesha haja ya kuwa na mfumo wa uwekezaji unaobainisha maeneo ya uwekezaji kati ya mashirika ya umma ya kibiashara na sekta binafsi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
“Lazima tuwe na sekta ya umma iliyoandaliwa kuwezesha na kufanikisha biashara na uwekezaji.l Kwa kufanya hivyo tutakuwa na sekta binafsi shindani, thabiti, jumuishi na inayowajibika katika uchangiaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” inasema sehemu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Ili kuwa na sekta imara ya kibiashara kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ya kisera, kiutawala na kiutendaji yatakayoainisha kwa uwazi sekta za kimkakati kwa ajili ya uwekezaji wa mashirika ya umma ya kibiashara, na hivyo kutoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza kwa upana zaidi katika maeneo mengine.”
Ili hili litimie lazima kukumbatia utumishi wa umma unaotambua umuhimu na kuunga mkono maendeleo ya sekta binafsi, kwa kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji.
Matarajio ni Tanzania kuwa moja kati ya nchi tatu zinazoongoza Afrika kwa kuvutia uwekezaji na urahisi wa kufanya biashara.
“Sekta imara ya biashara ni muhimu katika kukuza uchumi imara, jumuishi na shindani,” inasema sehemu ya Dira.
“Kuwepo kwa biashara ndogo, za kati na kubwa zinazomilikiwa na wafanyabiashara wa ndani na wa kigeni, pamoja na mashirika ya umma ya kibiashara, kunaimarisha ushiriki wa nchi katika soko la kimataifa.”
Sanjari na faida hizo, kutachochea ubunifu, utulivu na ustahimilivu wa kiuchumi na kuhakikisha ukuaji endelevu wa biashara unaoendana na mabadiliko ya soko.