Na Hellen Mtereko,Mwanza
Timu ya wataalamu na madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imetoa elimu ya afya hususan ugonjwa wa saratani kwa askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza katika uwanja wa Polisi Mabatini.
Elimu hiyo imetolewa leo Jumatano Julai 16, 2025, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya saratani, dalili zake na njia za kujikinga.
Elimu hiyo imetolewa na jopo la wataalam wa afya wakiongozwa na Dk Getrud Mashasha, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani ambaye amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani Kanda ya Ziwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu, shughuli za uchimbaji madini, mabadiliko ya hali ya hewa, kuzaa katika umri mdogo, na wanaume kutofanyiwa tohara.
Pia, ametoa wito kwa jamii hususan Jeshi la Polisi kuzingatia afya ya akili, kufanya tohara, kuepuka ngono zembe na mienendo mibaya ili kudhibiti maambukizi ya saratani.
Aidha, Dk Mashasha ametangaza uzinduzi wa mbio za hisani maarufu ‘Bugando Health Marathon’ Msimu wa Pili, zitakazofanyika Agosti 03, 2025, kwa lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia matibabu ya saratani kwa wagonjwa hospitalini hapo.
Mbio hizo zitakuwa na kaulimbiu inayosema: “Kimbia, Changia Matibabu ya Saratani”.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mabatini Mrakibu wa Polisi, Steven Kisaka ameomba ushirikiano zaidi kati ya Hospitali ya Bugando na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu ya afya kwa askari na familia zao.
Ombi hilo limepokelewa na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Bugando, Dk Samson Kichiba, aliyeahidi kulifikisha kwa uongozi wa hospitali ili kuweza kutoa huduma ya pamoja.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa, wakaguzi na askari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, amepongeza juhudi hizo na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litashiriki kikamilifu katika tukio hilo la kijamii kwa lengo la kusaidia jamii na kuonesha mshikamano.