

Mkurugenzi wa Uvuvi Profesa Mohamed Sheikh akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo, Julai 16, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua wa mkutano wa wadau wa sekta ya uvuvi ulioandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa lengo la kukuza uelewa wa pamoja kuhusu uhusiano wa haki za binadamu na usimamizi wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo.

Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Bw. Mohamed Khamis Hamad akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta ya Wavuvi wadogo.


Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka wa THBUB, Bi. Jovina Muchunguzi akitoa mada katika mkutano wa wadau wa sekta ya Wavuvi wadogo.


Mshauri wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark Bi. Sofie Hansen akitoa mada katika mkutano wa wadau wa sekta ya wavuvi wadogo.

Mwakilishi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Wakili Deogratius Bwire akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta ya wavuvi wadogo.

Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Mohamed Sheikh akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wakiwemo Maafisa Uvuvi pamoja wavuvi wadogo kutoa mikoa mbalimbali nchini.






Picha za matukio mbalimbali.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa sekta ya uvuvi na mifugo, imetakiwa kuendelea kufanya tafiti na kuzifanyia kazi ili kuleta matokeo chanya kwa Taifa, hususan katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali za uvuvi na uzingatiaji wa haki za binadamu.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo, Julai 16, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa sekta ya uvuvi, Mkurugenzi wa Uvuvi Profesa Mohamed Sheikh amesema kuna umuhimu mkubwa wa kufanya tafiti na kuzifanyia kazi ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta hiyo.
Profesa Sheikh amewakumbusha wavuvi nchini kuzingatia wajibu wao katika kudai na kutekeleza haki zao za msingi.
“Huwezi kudai haki bila kutimiza wajibu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 26 na 27, inaeleza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kulinda rasilimali za nchi. Haki huenda sambamba na wajibu. Hivyo tunapozungumzia haki za wavuvi, ni vyema pia tukasisitiza wajibu wao,” amesema Profesa Sheikh.
Amesisitiza umuhimu wa washiriki wa mkutano huo kutoa maoni na mapendekezo yanayojikita katika sheria, sera, miongozo na taratibu mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Bw. Mohamed Khamis Hamad, amesema kuwa changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo zinaweza kutatuliwa kupitia elimu kwa jamii za wavuvi ili kuongeza uelewa wa haki za binadamu na kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho yanayolenga kulinda haki za wavuvi wadogo.
“Utafiti umebaini changamoto mbalimbali katika sekta ya uvuvi, ikiwemo unyanyasaji wa wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na matatizo ya fidia kwa wavuvi wanaopisha uwekezaji katika maeneo yao ya kazi. Ni muhimu kuheshimu haki za watu pamoja na shughuli zao, kwani biashara yoyote haiwezi kuendelea pasipo kufanya hivyo,” amesema Bw. Hamad.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka wa THBUB, Bi. Jovina Muchunguzi, amesema mkutano huo umewashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo wavuvi wadogo kutoka mikoa ya Tanga, Mtwara, Lindi na Dar es Salaam, kwa lengo la kuangazia haki za binadamu zinazohusiana moja kwa moja na masuala ya bahari na ustawi wa wavuvi wadogo.
Bi. Muchunguzi amesema tume imefanya uchambuzi wa awali kuhusu haki za wavuvi wadogo katika ukanda wa Pwani na kubaini changamoto mbalimbali, hasa katika usimamizi na upatikanaji wa rasilimali za bahari, ambapo imebainika kuwa wavuvi wengi wanakabiliwa na ugumu wa kuzifikia rasilimali hizo kwa ufanisi.
Nao washiriki wa mkutano huo, akiwemo Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Bi. Habiba Idd Athumani, pamoja na Mwakilishi wa Wavuvi kutoka Wilaya ya Mkinga, Bw. Kassimu Abdallah, wamewashukuru waandaaji wa mkutano huo kwani kuna manufaa makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika kuanzia Julai 16 hadi 17, 2025 jijini Dar es Salaam, umeandaliwa na THBUB kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa lengo la kukuza uelewa wa pamoja juu ya uhusiano wa haki za binadamu na usimamizi wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo. Pia mkutano huo utajadili kwa kina changamoto mbalimbali na kupendekeza mbinu bora za kuzitatua.