Na John Bukuku, Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, amesema kuwa uwepo wa dawa mbalimbali bandia na duni nchini ni hatari sana kwa afya za wananchi.
Ameyasema hayo leo Julai 16, 2025, wakati akifungua kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari kutoka mikoa mbalimbali kinachofanyika katika hoteli ya JB mjini Tabora.
Mhe. Chacha amepongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa juhudi zake katika kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Aidha, amewataka wanahabari kuendelea kuwaelimisha wananchi na umma kwa ujumla kupitia kalamu na sauti zao kuhusu uwepo wa dawa mbalimbali bandia na duni hapa nchini, kwa kuwa jamii ina imani kubwa nao.
Pia, ametoa rai kwa wafanyabiashara kuacha kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi visivyo salama.
Kwa upande mwingine, Mhe. Chacha amesema kuwa kupitia vyombo vya habari, jamii imeweza kufahamu TMDA na kazi zake, sambamba na kutoa taarifa wanapotilia mashaka ubora na usalama wa bidhaa.
Amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali inaongoza juhudi za kudhibiti bidhaa bandia na kuhimiza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka maeneo rasmi.
Aidha, amesema serikali kupitia TMDA haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaouza bidhaa bandia na zisizo salama kwa watumiaji, kwani afya ya Watanzania ni kipaumbele kikuu cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho. Alieleza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kutoa elimu kwa wahariri kuhusu majukumu ya TMDA, mafanikio yaliyopatikana, na mikakati ya kuimarisha usalama wa bidhaa zinazotumika nchini.
Dkt. Fimbo alisema kuwa TMDA inasimamia sheria mbili kuu: Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219, na Sheria ya Wakala za Serikali, Sura 245. Kupitia sheria hizo, TMDA inawajibika kudhibiti dawa, vifaa tiba, vitendanishi, vipodozi, chakula pamoja na bidhaa za tumbaku kabla ya kuingia sokoni.
Ameongeza kuwa kwa sasa TMDA imeboresha mifumo yake kwa asilimia 100 kwa njia ya kidijitali, huku huduma nyingi zikitolewa mtandaoni ndani ya saa 24, ikiwemo usajili wa bidhaa, utoaji wa vibali na ukaguzi wa bidhaa sokoni.
Dkt. Fimbo alitaja pia mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa watumishi kutoka 278 hadi 439, kuanzishwa kwa viwanda 18 vya dawa na vifaa tiba nchini, ujenzi wa maabara tatu za kisasa na utoaji wa gawio la zaidi ya Shilingi bilioni 23 kwa Serikali.
Kikao kazi hicho kimewakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari na kinatarajiwa kuendelea kwa siku ya pili, kwa kuwahusisha waandishi wa habari wa mikoa ya Kanda ya Magharibi. Mafunzo hayo yatajikita katika namna ya kuripoti kwa usahihi habari za afya na udhibiti wa bidhaa hatarishi.