Na Fauzia Mussa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeendesha mafunzo maalum kwa waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao katika ngazi ya jimbo, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani Mjini Unguja, yakiwakutanisha watendaji 105 kutoka mikoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini na Kusini Unguja, huku mada 12 muhimu zikiwasilishwa kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kina juu ya taratibu na sheria za uchaguzi.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk, aliwataka washiriki kuhakikisha wanasoma kwa makini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi ili kuepuka kukiuka maelekezo ya tume.
“Uchaguzi ni mchakato wa kikatiba na kisheria. Zipo hatua mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, amani na wa kuaminika,” alisema Jaji Mbarouk.
Alisisitiza kuwa uteuzi wa wasimamizi hao umefanywa kwa kuzingatia masharti ya sheria ya uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024 pamoja na ibara ya 74 (6) ya Katiba, ambayo inaitambua Tume kama chombo pekee cha kusimamia na kuratibu uchaguzi wa Rais na Wabunge.
Aidha, aliwakumbusha washiriki kuwa tangu siku ya uteuzi wao, wanakuwa ni watumishi wa Tume na si wa mamlaka nyingine, na kwamba uwajibikaji wao unatakiwa kuelekezwa kwa Tume hiyo pekee, isipokuwa kama kuna maelekezo yanayotolewa kwa mujibu wa sheria nyingine za nchi.
Akisisitiza juu ya maadili ya kazi, Jaji Mbarouk aliwataka watendaji wa uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa uadilifu, uzalendo, uwazi na bila upendeleo.
Alionya dhidi ya ajira za upendeleo kwa ndugu au jamaa wasiokuwa na sifa, akisema uchaguzi unahitaji watu wenye weledi na wachapakazi.
“Epukeni kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa au wadau wa uchaguzi. Zingatieni Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya Tume kwa kila hatua,” alisisitiza.
Alihimiza umuhimu wa kuwashirikisha wadau wote wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria, katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na sheria.
Sambamba na hayo, alieleza umuhimu wa kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema, ili kubaini mahitaji yake maalum na kuweka mpangilio mzuri unaowezesha uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.
Vile vile aliwataka kusimamia viapo vyao vya kutunza Siri na kujitoa au kutokuwa mwanachama wa Chama chochote cha siasa kipindi chote cha uchaguzi .
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ofisi ya Zanzibar, Adam Juma Mkina, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwapa watendaji wa uchaguzi uelewa wa taratibu za uchaguzi na kuwajengea uwezo wa kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria na Katiba.
“Tunaamini baada ya mafunzo haya, watendaji wataweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya kisheria,” alisema.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa wakati mmoja pia katika mikoa ya Morogoro, Mtwara, Tabora, Geita na Kilimanjaro, ambapo washiriki wanapata nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mafanikio makubwa.
Tume imeeleza kuwa mchakato mzima wa maandalizi ya uchaguzi unaendelea kufanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa haki, huru na wa kuaminika kwa Watanzania wote.