Mbunge wa Muleba Prof.Anna Tibaijuka akiongea na watumishi wa kituo cha afya wakati wa ziara ya katibu mkuu
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula akiongea na watumishi wa kituo cha afya kaigara(hawapo pichani)wakati wa ziara yake wilayani muleba.Kushoto ni Mganga Mkuu wa Wilaya Muleba Dkt. Modest Burchard
Katibu Mkuu Dkt.Zainab Chaula akiwasalimia wananchi waliofika kupata huduma kwenye kituo cha afya,ambapo aliwahamasisha akina mama kuwapatia chanjo zote watoto wao
Wakazi wa Muleba waliofika kwenye kituo cha afya kaigara waliofika kupata huduma kwenye kituo hicho.
********************************
Na. Catherine Sungura-Muleba
Wananchi wametakiwa kuwa na bima ya afya ili kuweza kupata matibabu kwani ugonjwa hauchagui saa wala siku.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula wakati alipotembelea kituo cha afya kaigara kilichopo wilayani hapa wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye mkoa wa kagera inayoshirikisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
“Ugonjwa hauna siku wala saa hivyo nimepita hapa kuwahamasisha ili muweze kupata matibabu wakati wote na sehemu yoyote ni vyema mkawa na bima ya afya ,na sasa hivi NHIF imekuja na vifurushi vipya vya viwango mbalimbali ambavyo kila mwananchi hapa anaweza kumudu kwani mna ardhi nzuri hivyo kila mmoja akipanda migomba na akauza anaweza kukata bima hizo”.Alisisitiza Dkt. Chaula
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu huyo alitoa elimu kwa wananchi hao waliofika kupata huduma kwenye kituo hicho cha afya juu ya kuwalisha watoto wao vyakula mchanganyiko pamoja na kunyonyesha watoto kwa muda wa miaka miwili.
“Hawa watoto wetu ndio askari na viongozi wetu wa baadae ,makuzi ya mtoto yapo katika kipindi cha utoto kuanzia siku hadi miaka mitano hivyo hakikisheni mnawalisha vyakula mchanganyiko,kukaa nao karibu na kuwapatia chanjo zote”.Alisema
Aidha, alisema hali ya lishe kwa mkoa wa kagera bado sio nzuri kwani ni asilimia 38.9 hivyo aliwata watoa huduma kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na lishe bora ili kuimarisha lishe kwa watoto.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za tiba wizara ya afya Dkt. Grace Magembe aliwataka akina baba wilayani hapo kuwa na mazoea ya kuwasindikiza wake zao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwani malezi ya mtoto ni ya baba na mama,hivyo baba akishiriki kwenye malezi anakuwa ni msaada mkubwa na kumfanya mama kufanya kazi zingine.
Wakati huo huo Mkurugenzi msaidizi huduma za ustawi wa jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Rasheed Maftah aliwahimiza waganga wakuu wa wilaya kusimamia uwajibikaji kwa kuhakikisha kwamba kamati za afya zinashirikishwa katika kusimamia rasilimali dawa ili kuzuia uvujaji na wizi wa dawa.
Vilevike Maftah aliwahimiza akinamama wajawazito kuwahi kuhudhuria mapema kliniki pale anapohisi ni mjamzito ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi
Hata hivyo aliwakumbusha waganga wakuu kuunda na kuhuisha kamati za afya za vituo na kuhakikisha zinafanya kazi ili kuimarisha ubora za huduma za afya na ustawi wa jamii kwa wananchi.