Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
Gazeti la The Citizen na Mwananchi yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), yamelazimika kuomba radhi kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Kyando Mchechu, kufuatia makala iliyoandikwa na kuchapishwa na gazeti hilo tarehe 23 Machi 2018.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia hukumu iliyotolewa tarehe 3 Machi 2023 na Jaji Leila Mgonya, kubaini kuwa taarifa hiyo haikuwa na ukweli, haikuungwa mkono na ushahidi wowote, na ililenga kumchafua Mchechu kwa nia ovu.
Katika makala hiyo ya mwaka 2018, Mchechu alituhumiwa kwa madai ya kushiriki vitendo vya rushwa na kuingia mikataba ya upendeleo binafsi akiwa katika nafasi yake ya uongozi ndani ya NHC. Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa madai hayo yalikuwa ya uongo na yalimhusisha kwa njia isiyo halali, jambo lililosababisha madhara makubwa ya kiutu na kijamii kwa Mchechu.
Mahakama iliagiza gazeti hilo kuchapisha radhi rasmi na kujiondoa kwa maandishi makosa yote yaliyofanyika, ikiwa ni pamoja na kuchapisha radhi hiyo kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti hilo kwa ukubwa ule ule wa makala iliyomhusu Mchechu.
Aidha, Mahakama iliiamuru Mwananchi Communications Limited pamoja na mhariri wa gazeti hilo kumlipa Mchechu fidia ya Shilingi Bilioni 2 kwa kumchafulia jina, pamoja na Shilingi Milioni 500 kwa hasara aliyoipata. Pia, waliamriwa kulipa riba ya asilimia 12 ya kiasi hicho kuanzia Machi 2023 hadi malipo yatakapokamilika.
Jitihada za Mwananchi Communications kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani hazikuzaa matunda, kwani tarehe 4 Juni 2025, Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa hiyo na kuidhinisha hukumu ya Mahakama Kuu, ikisisitiza kuwa uandishi wa habari unapaswa kuzingatia ukweli, uwajibikaji na ustaarabu.
Kwa sasa, The Citizen imechapisha radhi rasmi kwa Mchechu, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mahakama. Radhi hiyo imeeleza kuwa taarifa za awali hazikuwa za kweli na gazeti hilo limejifunza kutokana na tukio hilo kwa kuahidi kuwa makini zaidi katika uchapishaji wa habari na kuimarisha imani ya wananchi katika taasisi za sheria na haki