Na Silivia Amandius, Bukoba – Kagera
Katika kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita kuhakikisha Watanzania wote wanatazamiwa kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza rasmi zoezi la kugawa majiko na mitungi ya gesi kwa watumishi wa Magereza yote ya mkoa wa Kagera.
Zoezi hilo limezinduliwa katika Gereza la Bukoba ambapo jumla ya watumishi 99 wamenufaika na vifaa hivyo. Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Lucas Charles, wakati wa uzinduzi huo, amesema kuwa serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha magereza yote nchini pamoja na watumishi wake wanatumia nishati safi ya kupikia kama sehemu ya ajenda ya kitaifa ya kulinda afya na mazingira.
Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha kila Mtanzania – awe mjini au kijijini – anakuwa sehemu ya mapinduzi ya matumizi ya nishati salama, huku REA ikihamasisha watumishi wa umma kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Kwa upande wake, Emmanuel Yesaya, Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kutoka REA, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, alibainisha kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 35 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo nchi nzima. Kiasi hicho kitatumika kwa ujenzi wa miundombinu ya nishati safi kwenye magereza yote, ugawaji wa jumla ya tani 850 za mkaa mbadala, ununuzi wa mashine 61 za kuzalisha mkaa huo, pamoja na kusambaza mitungi na majiko ya gesi kwa watumishi wote wa Jeshi la Magereza.
Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi yatapunguza kwa kiasi kikubwa athari za kimazingira, kuimarisha afya ya watumishi, na kuongeza muda wa uzalishaji kwa kuwaondolea changamoto ya kutumia muda mrefu kutafuta kuni au kusubiri moto wa mkaa.a p
Naye Kamishna Msaidizi wa Magereza anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, Heron Noberth, alisema kuwa magereza yote mkoani humo yameanza rasmi kutumia nishati safi ya kupikia tangu Januari 2025 baada ya kusaini mkataba na serikali.
Ameeleza kuwa hatua hiyo imepunguza gharama kubwa zilizokuwa zikitumika katika ununuzi wa mafuta na uchukuaji wa kuni, hali iliyokuwa ikiweka hatarini usalama wa maafisa na wafungwa waliokuwa wakipelekwa kuchukua kuni misituni.
Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi yameleta mabadiliko makubwa katika maisha ya kila siku ya watumishi na familia zao, na kutoa rai kwa walionufaika kuwa mabalozi wa mabadiliko hayo kwa jamii inayowazunguka.