Na John Bukuku, Dar es Salaam
Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) imechukua hatua madhubuti kuimarisha uelewa wa sheria za ushindani miongoni mwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kuzindua kliniki maalum ya biashara katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba.
Kupitia kliniki hiyo, FCC inalenga kuwapatia wafanyabiashara hawa taarifa sahihi na za faragha kuhusu sheria za ushindani na ulinzi wa watumiaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha ukuaji shirikishi wa uchumi unaozingatia usawa na haki katika soko.
Akizungumza Julai 4, 2025 katika banda la FCC viwanja vya Sabasaba, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Hadija Ngasongwa alisema kuwa taasisi hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya washiriki 3,500 kutoka sekta mbalimbali za biashara ili kuwajengea uelewa utakaowawezesha kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria, huku wakijilinda dhidi ya ushindani usio wa haki.
“Kwa kliniki hii, tunawawezesha wajasiriamali wa kati na wadogo kuelewa haki zao kama watumiaji wa soko, lakini pia wajue wajibu wao kisheria. Hii ni hatua muhimu kwa ukuaji wao na mchango wao katika uchumi wa taifa,” alisema Bi. Ngasongwa.
Aliongeza kuwa FCC imekuwa ikiendesha kampeni mbalimbali za uelimishaji, pamoja na kufanya tafiti na ufuatiliaji wa mwenendo wa soko ili kudhibiti bidhaa bandia na uonevu wa kibiashara unaoweza kudhoofisha juhudi za wajasiriamali chipukizi.
Kwa mujibu wa Bi. Ngasongwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya kibiashara kwa kuweka mifumo rafiki kwa wawekezaji, hatua inayochochea ukuaji wa sekta binafsi hususan kwa vijana na wanawake wanaoingia kwenye biashara.
“Sheria zetu ni rafiki kwa wawekezaji na kwa wajasiriamali wanaochipukia. Tunataka kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi bila vikwazo vya ushindani usio wa haki,” alisisitiza.
Bi. Ngasongwa alieleza kuwa FCC haijajikita tu katika kudhibiti ushindani usio halali kutoka kwa makampuni makubwa, bali pia inaweka nguvu katika kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani kujijengea uwezo wa kukuza biashara zao kwa njia ya haki, ili hatimaye waweze kushindana kitaifa na kimataifa.
Alihitimisha kwa kusema kuwa FCC itaendelea kuwa karibu zaidi na jamii ya wafanyabiashara kupitia majukwaa ya wazi kama Sabasaba, ili kuhakikisha elimu, msaada na usimamizi wa sheria unapatikana kwa wote kwa wakati.