Ingirito-Lindi
Chama Cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali Tanzania – TAGCO, kimeshishiriki mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano ya Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Nurdin Ndimbe yaliyofanyika Kijijini kwao Ingirito, Wilayani Kilwa Mkoani Lindi.
Akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya uongozi wa TAGCO na wanachama wake, mwakilishi wa Chama hicho ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Halmashauri ya Mji Rufiji Bw. Emmanuel Kapandila alisema kuwa Nurdin Ndimbe alikuwa mwanachama mtiifu wa TAGCO na mtumishi mwenye weledi mkubwa , aliyejali misingi ya kazi na tasnia ya mawasiliano na kuwa TAGCO imeondokewa na hazina kubwa.
“TAGCO tumeondokewa na mtaalam mbobevu aliyesimamia maadili ya taaluma yake na mcha Mungu. Nurdin alikuwa mtu mwema, rafiki wa kila mtu na mwenye mchango uliotukuka katika jamii, hakika ametuachia alama itakayotufanya tuendelee kumkumbuka kila wakati”.
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, Msemaji wa familia na Kaka wa Marehemu, aliishukuru TAGCO kwa michango na kushiriki wakati wa msiba mpaka mazishi.
Marehemu Nurdin Ndimbe alizaliwa Aprili 13, 1966 kijijini Ingirito, Kata ya Chumo Wilaya ya Kilwa na kufanya kazi katika Wizara ya Maji, Mahakama Kuu na baadaye Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo umauti ulimkuta Juni 30,2025 na kuzikwa Julai 2, 2025 Kijijini kwao Ingirito.