Dar es Salaam
Wananchi wametakiwa kufika katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, ili kupata huduma za kisheria na elimu kuhusu masuala mbalimbali ya sheria.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Neema Ringo, wakati wa maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Bi. Ringo amesema kuwa kwa mara ya kwanza, ofisi hiyo inashiriki maonesho hayo kama taasisi huru, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakishiriki kupitia banda la Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Kwa mwaka huu tumeona ni muhimu kuwa na banda letu ili kuwa karibu zaidi na wananchi kwa kuwapatia huduma na kuwaelimisha kuhusu majukumu tunayoyatekeleza,” alisema Ringo.
Aidha, alieleza kuwa ofisi hiyo imekuja na machapisho mbalimbali yanayotoa elimu ya kisheria, huku pia kukiwa na eneo maalum la kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, ajira na matatizo mengine ya kisheria.
“Tutaendelea kutoa huduma hizi kwa wananchi hadi mwisho wa maonesho haya, na tunawahimiza wote wenye changamoto za kisheria kufika banda letu kwa ajili ya kupata msaada,” alisisitiza.
Akizungumzia mabadiliko ya sheria, Bi. Ringo alikumbusha kuwa mwezi Aprili mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alizindua Juzuu Mpya za Sheria zilizofanyiwa marekebisho, ambazo zimeanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025.
“Juzuu hizo mpya za mwaka 2025 zimechukua nafasi ya zile za mwaka 2002 ambazo sasa hazitumiki tena. Wananchi wanaweza kuzipata hapa katika banda la Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria,” alieleza Ringo.
Alisisitiza kuwa lengo kuu la ushiriki wao katika maonesho haya ni kutoa huduma kwa wananchi na kuwawezesha kupata uelewa wa masuala ya kisheria yanayowahusu moja kwa moja.