Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa mpira wa miguu wakati wa ufunguzi wa mashindano ya mkuu wa majeshi yaliyofanyika Julia 2, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax akikagua timu ya mpira wa miguu katika mashindano ya mkuu wa majeshi wakati wa ufunguzi yaliyofanyika Julia 2, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
…………
NA NOEL RUKANUGU, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax, amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuendeleza Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025), ambayo yanatoa fursa ya kukuza vipaji na kuimarisha timu za jeshi hilo zitakazoshiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza Julai 2, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Waziri Dkt. Stergomena Lawrence amesema kuwa michezo hiyo ni jukwaa muhimu la kuibua na kuendeleza wanamichezo ndani ya JWTZ, sambamba na kuongeza idadi ya wanamichezo wenye uwezo wa kushindana katika viwango vya juu.
Dkt. Lawrence amesisitiza kuwa michezo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha, ametoa pongezi kwa uongozi wa JWTZ chini ya Jenerali Jacob Mkunda kwa kuendeleza mashindano haya tangu yalipoanzishwa mwaka 2014.
“Mashindano haya yanaunga mkono kwa vitendo dhamira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kukuza na kuimarisha michezo nchini. Sote tumeshuhudia jitihada zake za dhati katika sekta ya michezo,” amesema Dkt. Lawrence.
Waziri huyo pia ametoa wito kwa taasisi na mashirika mbalimbali kuanzisha programu za kukuza vipaji katika sekta ya michezo. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutumia haki ya kikatiba ya kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaoendeleza amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, amesema kuwa kuendeleza mashindano hayo kunatokana na faida nyingi wanazopata wanajeshi kupitia ushiriki wao katika michezo.
Ameeleza kuwa baadhi ya faida hizo ni pamoja na kuimarisha afya ya mwili kwa kuongeza nguvu, mwepesi na uvumilivu; pamoja na afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na kuchochea uzalishaji wa homoni za furaha.
Aidha, michezo huongeza mshikamano na uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja, jambo ambalo ni muhimu hasa wakati wa vita, na pia huongeza ushindani, nidhamu na ufanisi katika mafunzo ya kijeshi.
“Michezo huimarisha mahusiano ya kijamii na kidiplomasia, ikiwemo michezo ya Afrika Mashariki. Hivyo basi, michezo si burudani tu bali ni nyenzo ya mafunzo, afya, mshikamano na mafanikio ya kijeshi,” amesema Luteni Jenerali Othman.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wadhamini mbalimbali wa mashindano hayo, akiwemo Kampuni ya Azam Media kwa kurusha matangazo mubashara ya mashindano ya Mkuu wa Majeshi yanayoshirikisha michezo mbalimbali.
Mashindano hayo ya Mkuu wa Majeshi yatashirikisha michezo mbalimbali kwa wanaume na wanawake ni pamoja na mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, ngumi, mieleka, kuruka vikwazo, kuogelea, vishale, golfu na shabaha.
Mashindano hayo yatatumia viwanja mbalimbali kulingana na aina ya mchezo, hivyo Uwanja wa Azam Complex utatumika kwa mechi ya mpira wa miguu siku ya ufunguzi na kufunga mashindani hayo.
Viwanja vya Kambi ya Generali Twalipo – Mgulani vitatumika kwa michezo ya mpira wa kikapu, netiboli, mikono, wavu, ngumi, mieleka na kuruka viunzi.
Viwanja vya Lugalo Golf Club vitatumika kwa mchezo wa golfu, fukwe za Msasani zikitumika kwa mchezo wa vishale, huku michezo ya kuogelea itafanyika Makao Makuu ya Kamandi ya Wanamaji.