Katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua na kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia katika sekta ya fedha, Benki ya NMB imetambulisha mashine ya ATM maalum inayomwezesha mteja kuweka fedha moja kwa moja kwenye akaunti yake bila kupitia kwa mhudumu.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba), Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya NMB, Bw. Seka Urio, amesema lengo la ubunifu huo ni kuwasaidia wafanyabiashara wanaoshiriki maonesho hayo kutotembea na fedha taslimu. Kwa njia hiyo, wanapata urahisi wa kuweka fedha zao moja kwa moja kwenye akaunti kupitia ATM hizo maalum.
“Tunataka kuwapa urahisi wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla waweze kuweka fedha zao muda wowote bila kwenda dirishani. Hii ni sehemu ya mkakati wa NMB kuhakikisha huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi na usalama zaidi,” alisema Bw. Urio.
Kuhusu usalama wa miamala hiyo, Bw. Urio alieleza kuwa ATM zote za NMB zina ulinzi wa kutosha, ikiwa ni pamoja na uwepo wa walinzi na kamera maalum zinazorekodi matukio yote yanayotokea katika eneo la mashine hizo.
“Tumejipanga kuhakikisha mteja anapoweka fedha anakuwa salama. Kuna kamera za ulinzi na walinzi wa kutosha kuhakikisha mazingira ni salama muda wote,” aliongeza.
Huduma hii ya ATM za kuweka fedha (Cash Deposit ATMs) inatarajiwa kuwa suluhisho la kisasa linalochochea ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi wengi zaidi.