Na Silivia Amandius, Missenyi
Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za Green Acres Tanzania zilizopo Missenyi na Dar es Salaam, Bi Jacklyne Siima Rushaigo, ameonyesha dhamira ya kulitumikia Taifa kwa kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Missenyi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bi Jacklyne, ambaye ana Shahada ya Uzamili katika masuala ya Benki na Fedha (MSc), amejitokeza kuwa mmoja wa wanawake wawili waliothubutu kuingia katika kinyang’anyiro hicho, kati ya wagombea 13 waliokwisha kuchukua fomu hadi sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejesha fomu katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Missenyi iliyopo Nyabihanga – Kyaka, Bi Jacklyne alisema ana uwezo, uelewa na maono ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
“Naamini nina sifa, uzoefu na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Missenyi kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kushirikiana nao bega kwa bega,” alisema
Ushiriki wa wanawake katika siasa unazidi kupanuka, na hatua ya Bi Jacklyne kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni mfano wa ujasiri wa wanawake wanaoamini katika mabadiliko chanya kwa jamii.