Mwenyekiti wa TAMSTOA Chuki Shaban (kulia) akirejesha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ilala Silvester Yared.
………….,
Na Sidi Mgumia, Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA), Chuki Shaban amechukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa mara baada ya kurejesha fomu hiyo Chuki amesema amechukua uamuzi huo kwa kuwa anaamini anaweza kusimamia utekelezaji wa ahadi zilizopo kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM 2025-2030 katika jimbo hilo ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta maendeleo kwa wakazi wa Segerea na Watanzania wote kwa ujumla.
Pamoja na hilo, amesema kuna changamoto ambazo wenzao waliotangulia wameshindwa kuzitatua, hivyo kwa moyo wa uzalendo, ujasiri na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi wa Seregerea amerejesha rasmi fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo hilo ili aweze kutatua changamoto zilizopo.
“Nina kiu ya kuhakiksha kwamba ninazisimamia na kuzitatua changamoto zilizopo ambazo ni pamoja na masuala ya maji, barabara na usalama wa mali zetu kama vile viwanja na mengineyo na niko tayari kushirikiana na wananchi kuharakisha maendeleo.
“Nitaomba idhini ya kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutimiza maono yake, na nitaomba ruhusa ya kuwawakilisha kikamilifu wakazi wa Segerea, ” ameahidi.