Na Silivia Amandius – Biharamulo, Kagera
Mwanasiasa mahiri na aliyewahi kuhudumu kama Mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa kipindi cha 2020–2025 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Ezra Chiwelesa, ameonyesha nia ya kuendelea na safari ya kisiasa kwa kuchukua rasmi fomu ya kugombea ubunge kwa awamu ya pili.
Hatua hiyo imekuja kama sehemu ya dhamira yake ya kuendeleza juhudi za maendeleo katika jimbo hilo, akisisitiza kuwa anaendelea kuwa na ari na moyo wa utumishi kwa wananchi waliomuamini kwa miaka mitano iliyopita. Chiwelesa amesema anarejea kwa nguvu mpya, maarifa mapya na mikakati madhubuti ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Biharamulo Magharibi.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika ofisi za CCM Wilaya ya Biharamulo, Mhandisi Chiwelesa alieleza kuwa uzoefu alioupata katika kipindi chake cha kwanza bungeni umemjengea msingi mzuri wa kuelewa kwa undani changamoto zinazowakabili wananchi na namna ya kuzitatua kwa ufanisi.
“Nina ndoto kubwa kwa Biharamulo Magharibi. Natamani kuona tunasonga mbele zaidi kwenye sekta za elimu, afya, miundombinu, na kilimo. Huu ni mwendelezo wa kazi tuliyoianza, na naamini bado wananchi wanahitaji mchango wangu,” alisema Chiwelesa kwa kujiamini.
Fomu hiyo alikabidhiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Biharamulo, Bw. Adam Soud, ambaye alimpongeza kwa uamuzi wake na kusisitiza kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama hicho unaendelea kwa uwazi, haki na amani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CCM Wilaya, hadi sasa jumla ya wagombea 11 wamechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Biharamulo Magharibi kupitia chama hicho, ishara ya demokrasia pana na ushindani wa kisiasa ndani ya chama.
Chama hicho kinatarajia kuendesha kura za maoni ili kumpata mgombea atakayeungwa mkono na wanachama wengi na hatimaye kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.