Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam — Mwanasiasa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tickey Kitundu, ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Kivule, huku akieleza dhamira yake ya kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za wananchi.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kitundu alisema amepata uzoefu wa utumishi wa umma kupitia nafasi yake ya awali kama Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Ilala, akitokea Jimbo la Ukonga katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano. Alisema kupitia nafasi hiyo alitekeleza majukumu kwa weledi na kusaidia kutatua kero mbalimbali za wananchi katika maeneo aliyoyawakilisha.
“Nimekuwa nikishirikiana na serikali kutatua changamoto za wananchi kwa kiwango ambacho diwani anatakiwa kufanya. Sasa ninaamini ninao uwezo mkubwa zaidi wa kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge,” alisema Kitundu.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa maamuzi ya kuligawa Jimbo la Ukonga na kuunda majimbo mawili, ambapo Jimbo la Kivule ni mojawapo, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kutokana na ongezeko la idadi ya wakazi.
“Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Jimbo hili lina wakazi wapatao 431,726. Kugawanywa kwa jimbo kutasaidia kufikia wananchi kwa ukaribu zaidi. Mimi ni mkazi wa Kivule, najua changamoto zao, kubwa ikiwa ni miundombinu ya barabara,” alisisitiza.
Tickey Kitundu alisema endapo Chama Cha Mapinduzi kitampa ridhaa ya kugombea na kwa kibali cha Mungu, atahakikisha anashirikiana kwa karibu na Rais Samia kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo jipya.
Amesisitiza kuwa dhamira yake inalenga kuendeleza kazi na misingi ya utu, akihitimisha kwa kaulimbiu yake: “Mama Samia Mitano Tena — Kazi na Utu.”