Na Silivia Amandius
Missenyi, Kagera.
Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Mhe. Florent Kyombo, ametangaza rasmi nia ya kuwania tena ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.
Hatua hiyo ameichukua leo, Juni 30, 2025, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea katika ofisi za CCM Wilaya ya Missenyi, akieleza kuwa bado ana mengi ya kuyatekeleza kwa manufaa ya wananchi wa jimbo hilo.
“Miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi, lakini nimefanya jitihada kubwa kuweka misingi ya maendeleo. Sasa tunahitaji kukamilisha tulichoanza,” amesema Kyombo mbele ya wanahabari.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo barabara, maji, afya na elimu, bado kuna kazi ya kufanya ili kukamilisha miradi aliyoianzisha, hivyo anaomba ridhaa ya wananchi kuendelea na safari hiyo.
Kwa mujibu wa Mhe. Kyombo, amesema alipokabidhiwa jimbo hilo kulikuwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na barabara zisizopitika, vituo vichache vya afya, upungufu wa huduma za maji na umeme, pamoja na hali duni ya miundombinu ya shule.
“Sasa maji yapo, barabara zinafunguka, shule zina madarasa bora, na vituo vya afya vinaendelea kujengwa. Wananchi wa Missenyi wenyewe ni mashahidi wa haya,” alieleza kwa msisitizo.
Kyombo amesema kuwa katika kipindi kijacho cha miaka mitano, atajielekeza zaidi katika kuinua uchumi wa jamii ya Missenyi, akisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu sasa yafuatwe na maendeleo ya kiuchumi yanayogusa maisha ya watu mmoja mmoja.
“Lengo ni kuhakikisha mwananchi wa kawaida ananufaika moja kwa moja na kazi iliyofanywa. Ni muda wa kuimarisha maisha ya watu wetu kupitia kilimo, ajira na fursa nyingine,” aliongeza.
Akihitimisha, Kyombo amewaomba wananchi wa Missenyi kumpa nafasi nyingine ya kuendelea na kazi aliyoianza, akieleza kuwa maendeleo hayajengwi kwa maneno bali kwa vitendo.
“Wananchi wa Missenyi wanapaswa kuchagua kazi, si maneno. Mimi si mtu wa hadithi, bali wa kazi. Nimerudi kuomba ridhaa, kwa sababu najua changamoto zetu na njia ya kuzitatua,” alisema kwa kujiamini.
Mchakato wa uchukuaji fomu kwa wagombea ndani ya CCM unatarajiwa kuendelea hadi wiki ijayo huku ushindani mkali ukitarajiwa katika baadhi ya majimbo mkoani Kagera, ikiwemo Missenyi.