Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi( aliyeketi mstari wa pili kulia), Bw. Benjamini Mlimbila akifuatilia kikao cha wadaawa cha kujadili usikilizaji wa mashauri yatakayosikilizwa kuanzia Juni 24 hadi Julai 31.
(Picha na Dhillon John na Magreth Kinabo)
……………………..
Na Lydia Churi-Mahakama
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi inatarajia kusikiliza jumla ya mashauri 43 katika kikao maalum (Session) kinachotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 24 Juni mpaka tarehe 31 Julai, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hayo yamezungumzwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi Mhe. Issa Maige katika kikao cha Wadaawa kuhusu usikilizwaji wa mashauri hayo kilichowahusisha Majaji, Naibu Wasajili, Mtendaji na wasaidizi wa kumbukumbu na mawakili.
Mashauri yatakayosikilizwa ni yanayohusu migogoro ya ardhi ambapo yanatarajiwa kusikilizwa na Waheshimiwa Majaji sita wa Mahakama hiyo wakiwemo Jaji Issa Maige, Jaji Dr. Modesta Opiyo, Jaji Julius Mallaba, Jaji Awadh Mohamed na Jaji Salma Maghimbi.
Pia Mhe. Jaji Issa Maige aliwataka Mawakili kuendelea kujifunza kusajili mashauri kielektroniki; lakini kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mafunzo yanayotolewa na Mahakama hususani yale yanayohusu matumizi ya mfumo wa kielekitroniki wa kusajili mashauri mahakamani (JSDS).
Awali, Afisa TEHAMA ya Mahakama hiyo Bw. Dhillon John alisema katika kusajili mashauri kwa njia ya kielekitroniki amekuwa akikutana na changamoto ambapo baadhi ya mashauri hukosa taarifa muhimu na sahihi jambo linalosababisha wateja kukosa baadhi ya haki zao.
Aidha, akifunga kikao hicho, Mhe. Maige aliwashukuru wajumbe wa kikao hicho hususan Mawakili kwa kutoa mchango wao katika kuboresha hali ya usikilizwaji wa mashauri na kuwataka kufika kwa wingi kwenye vikao hivyo pindi wanapotakiwa kufika.