Waziri wa Madini, Doto Biteko akitoa msimamo wa serikali juu ya mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu mara baada ya kusikiliza na kujadili hoja za pande zote. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon Msanjila.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao kilichokua kikijadili mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara Jijini Dodoma jana.
Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila akizungumza jambo wakati wa kikao kilichokua kikijadili mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara Jijini Dodoma jana.
Mlalamikaji Magere Mang’era akiwasilisha lalamiko lake mbele ya viongozi waandamizi wa wizara alipofika katika kikao hicho ili kutatua mgogoro baina yake na Joseph Ocheng Ndugu.
Joseph Ocheng Ndugu akionesha mipaka ya eneo lenye mgogoro baina yake na Magere Mang’era wakati wa kikao kilichofanyika jana tarehe 12/02/2020 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na mmoja wa wajumbe wakisubiri kuanza kwa kikao cha kutatua mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akimwonesha mlalamikiwa moja ya nyaraka yenye udhibitisho katika mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu wakati wa kikao cha kutatua mgogoro huo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon Msanjila.
fisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya akielezea hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro wa Irasanilo katika kikao kilichohusisha Viongozi Waandamizi wa Wizara, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara jijini Dodoma jana tarehe 12/ 02/2020
………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kutumia Ofisi za Wizara katika kufikisha changamoto zao badala ya kufikisha kero zao kwa viongozi wengine wa nchi na serikali wasio na dhamana ya kusimamia Sekta ya Madini, kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha utatuzi wa kero zinazowakabili.
Waziri Biteko aliyasema hayo jana tarehe 12 Februari 2020, wakati wa kikao kilicholenga kumaliza mgogoro baina ya wachimbaji wadogo Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu waliokuwa wakigombea umiliki wa eneo la mita 23 lililopo katika leseni ya Irasamilo Gold Mine iliyopo Buhemba Wilaya Butiama mkoani Mara.
Pamoja na hayo, Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wa Mkoa wa Mara kupunguza migogoro na kuwaeleza wizara yake inatamani kukutana nao kwa nia njema na si kwa lengo la kujadili na kutatua migogoro ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
“Wizara inashughulika na sekta ya madini nchi nzima, kama kila mchimbaji atataka kuleta malalamiko yake ofisini kwa waziri basi kazi hazitafanyika.” Tungefurahi kukutana nanyi kuwaeleza vitu mnavyotakiwa kuviboresha ili kuongeza mapato ni si kutatua migogoro, Biteko alisisitiza.
Aidha, Biteko ameutaka uongozi wa mgodi na uongozi wa wachimbaji wadogo ngazi za wilaya na mkoa (Marema) kuhakikisha kwamba amani inatawala kwa wachimbaji na kuwafanya wachimbaji wachimbe na kuzalisha kuliko kutengeneza migogoro isiyoisha inayochangia katika kurudisha nyuma maendeleo yao. “Wanaotafuta pesa hawatumii muda mwingi kugombana”, amesisitiza Biteko.
Baada ya kufikia hatma ya mgogoro huo na kumtaka Afisa Madini Mkazi Nyaisara Mgaya kusimamia haki katika eneo hilo kama kikao kilivyoafiki kuwa mwenye haki ya kupewa eneo hilo ni Magere Mang’era, Biteko aliwataka wajumbe walioshiriki kikao hicho kurudi Mara na kuendelea na shughuli za uzalishaji huku wakitunza amani na ushirikiano miongoni mwao.
Aidha, aliwataka kumtumia Afisa Madini Mkazi aliyepo katika eneo hilo kama mlezi lakini pia alimtaka Afisa huyo kuishi na wachimbaji hao vizuri na kudumisha ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliutaka uongozi wa Wachimbaji wadogo wa madini (Marema) kusimamia haki kwa wananchi waliowapa dhamana ya kuwaongoza ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara.
“Mkoa wa Mara umejaliwa kuwa na rasilimali madini nyingi, msigeuze neema hiyo kuwa chanzo cha migogoro na kutishiana maisha”, alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aliendelea kusema Neema ya Rasilimali madini inapogeuka na kuwa chanzo cha matatizo na migogoro inahuzunisha.
Aidha, Nyongo alizitaka pande zote kukubaliana na matokeo na kuwa maamuzi yaliyofikiwa yasiwe chanzo cha mgogoro mwingine, “naomba kabisa amani itawale”.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuheshimu maamuzi ya Serikali na kutokuifanya serikali kutumia gharama kubwa katika kutatua migogoro ya wachimbaji badala yake muda unaotumika kutatua migogoro utumike kukusanya mapato ya serikali.
“Tumeweka ofisi za madini mikoani ili kupunguza matatizo madogo madogo kuletwa wizarani hivyo mzitumie ofisi hizo na kuamini maamuzi yanayotolewa na viongozi katika mikoa yenu yanakuwa Baraka zetu”. Msanjila alisisitiza.
Prof. Msanjila aliwahakikishia wajumbe kuwa maamuzi yaliyofikiwa na Wizara ni sahihi na ya mwisho na kubainisha kuwa endapo hawakubaliani na maamuzi hayo basi wasingefika katika kikao hicho.
Profesa Msanjila alisisitiza kuwa, mlango sahihi wa kutatua migogoro katika sekta ya madini ni Wizara ya Madini vinginevyo ni kupoteza muda na rasilimali.
Kwa upande wa wajumbe walioshiriki kikao hicho wengi walikiri kuwa mwenye haki ya kupewa eneo lililokuwa na mgogoro ni Magere Mang’era na kwa Mamlaka aliyonayo Waziri aliamuru eneo lenye mgogoro apewe mlalamikaji na kuhitimisha mjadala juu ya mgogoro huo.