Wataalamu wa Sekta za Habari, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamepongeza maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Dodoma, wakieleza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutaimarisha mazingira ya michezo na kutoa fursa zaidi kwa wananchi, hususan vijana.
Wataalamu wametoa pongezi hizo Oktoba 2, 2026, walipotembelea eneo la ujenzi wa uwanja huo kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa pamoja na kujifunza namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyowekeza katika miundombinu ya michezo.
Wamesema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa katika kukuza na kuibua vipaji vya vijana, kuongeza fursa za ajira na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na michezo, sambamba na kuiwezesha Tanzania kuwa na miundombinu yenye uwezo wa kuandaa na kuendesha mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa.
Mbali na uwanja huo, wataalamu hao wametembelea pia ujenzi wa Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mji wa Serikali Mtumba, pamoja na Ofisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Idara ya Habari MAELEZO.

