Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, amesema hadi sasa washiriki zaidi ya 2,000 wamekwishajisajili kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Mheshimiwa Spika ameyasema hayo leo, Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha, ambako Mkutano huo utafanyika.
Amesema nchi 149 tayari zimethibitisha kushiriki Mkutano huo, huku nchi nyingine zikiendelea kutoa taarifa za ushiriki wao.
Kwa upande wa washiriki kutoka Tanzania, amesema jumla ya watu 147 tayari wamejregistri kwa ajili ya kushiriki Mkutano huo.
“Natoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha Mkutano wa IPU kufanyika Tanzania.
“Nafahamu watu wa Arusha ni wakarimu na wana uzoefu wa kupokea wageni, kwa kuwa ninyi ndiyo mnaowakilisha mkoani hapa. Tunataka wageni wajionee ukarimu wa Watanzania,” amesema.
Aidha, amewataka Watanzania kutumia fursa ya Mkutano huo kukuza na kuonyesha biashara zao, pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali, ikiwemo utalii, ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
“Natumie pia fursa hii kukuza na kuonyesha biashara zetu, changamkieni fursa mbalimbali, ikiwemo utalii, kuhakikisha uchumi unakua Arusha,” amesema.
Aidha, aliwashukuru waandishi wa habari kwa kuutangaza Mkutano huo tangu maandalizi yake yalipoanza hadi sasa, akisema wanapaswa kuendelea kuhakikisha Mkutano huo unaleta heshima kwa Tanzania.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuandika mambo mazuri yanayoitambulisha Tanzania, hasa katika sekta ya utalii.
“Kwa sasa sekta ya utalii inachangia asilimia 26 ya Pato la Serikali. Malengo yaliyopo ni kuhakikisha sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 45,” amesema.
Amesema Tanzania inaweza kufikia malengo hayo iwapo itaendelea kutangazwa kupitia ukarimu, upendo na mapokezi mazuri kwa wageni.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika mengine ya kimataifa yaliyopo Geneva, Uswisi, Balozi Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo zimepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa IPU.
Amesema sifa hizo zinapaswa kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo, pamoja na Bunge kwa kuandaa Mkutano huo.
“Mafanikio ya Mkutano huu ni jaribio la utayari wetu wa kuandaa mikutano mingine. Kama tumeweza kuandaa huu wa washiriki 2,000 na wengine watakuja, ni hatua muhimu,” amesema.
Ameongeza kuwa ni jukumu la Watanzania, hasa wananchi wa Arusha, kuhakikisha wageni wanaondoka nchini wakiwa na taswira nzuri ya Tanzania.
Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utafanyika Oktoba 5 hadi 9, 2026 katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

