Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson (kulia) mara baada ya kuwasili katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mwanga.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua uwekaji wa kumbukumbu za taarifa za jotoridi la jokofu la dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua kadi ya bima ya afya ngazi ya jamii iliyoboreshwa kutoka kwa mgonjwa aliyefika hospitali ya Wilaya ya Mwanga kupata huduma za afya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akionyesha alama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika dawa zote ambazo zinatolewa Serikali kwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Prof. Jummane Maghembe.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kulia) akifafanua jambo kwa watumishi wa Wilaya ya Mwanga (hawapo pichani) kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga Prof. Jumanne Maghembe akisema jambo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati wa Ziara ya Dkt. Ndugulile Wilayani Mwanga.
………………………………………………………………………………………………………….
Na WAMJW – Mwanga, Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameutaka uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kuandaa mkakati madhubuti utakaowawezesha kuwa na vipimo muhimu vya afya.
Dkt Ndugulile ametoa agizo hilo leo alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kujionea hali ya utoaji huduma na kubaini kuwa hospitali hiyo haina vipimo vya damu, vipimo vya kemia pamoja vipimo vya CD4.
”Kwa miaka miwili sasa hakuna vipimo vya msingi katika hospitali hii, tunawakosesha huduma wananchi” amesema Dkt. Ndugulile
”Haiwezekani Hospitali kubwa ndani ya Wilaya kukosa vipimo vya msingi, haiwezekani mtu hapa sasa hivi anahitaji kipimo cha damu atoke hapa aende Hospitali ya Mawenzi Moshi kwa ajili ya vipimo” amesema Naibu Waziri Ndugulile.
Katika hatua za kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, Waziri Ndugulile ameushauri uongozi wa afya ndani ya Wilaya kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kununua vifaatiba hivyo ili wananchi waweze kupata huduma za vipimo ndani ya Wilaya ya Mwanga.
Aliendelea kushauri kuwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wao wanatoa mkopo wa majengo na vifaa kwa taasisi za umma na binafsi, mnaweza kuwafikia NHIF na kujadili kuhusu suala hili.
”Huko kwingine wanazitumia hizo fursa, kaeni na watu wa NHIF, Meneja wa NHIF kaa na viongozi wa Hospitali hii ikiwezekana mkubaliane hivyo vitu vipatikane kwa haraka” ameshauri Dkt. Ndugulile.
”Naamini mna wadau wa maendeleo ambao mnashirikiana nao katika mambo mbalimbali, timu ya afya ndani ya mkoa, wilaya pamoja na hospitali nawaombeni sana tuwe tunaomba vitu ambavyo vina manufaa kwa wananchi” amesisitiza Dkt. Ndugulile.
Awali akitoa salamu za wananchi wa Wilaya ya Mwanga, Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe amesema kuwa changamoto ya kijiografia ndani ya Wilaya hiyo inachangia wananchi kukimbilia hospitali za Wilaya jirani ili kuweza kupata huduma.
”Wilaya yetu hii ina upande wa mlimani na huku tambarare, wananchi wengi walio huku tambarare wanaona ni bora kwenda Moshi kwa ajili ya matibabu kuliko kwenda juu mlimani iliko Hospitali” amesema Prof. Maghembe.
Hata hivyo Prof. Maghembe amesema kuwa tayari ndani ya Wilaya wameshaanza taratibu za kujenga Hospitali nyingine eneo la chini (tambarare) ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waweze kupata huduma za afya ndani ya Wilaya ya Mwanga.