Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kinaendelea kuhuisha mitaala yake ili kukidhi mabadiliko ya uhitaji wa soko kwa kuandaa wataalam wa sekta ya Ardhi kwa maendeleo ya chuo na taifa kwa ujumla.
Mitaala inayohuishwa katika chuo hicho inahusisha masomo ya Urasimu Ramani; Usimamizi wa Ardhi, Uthamini na Usajili pamoja na Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji ambayo mitaala yao ilipitishwa na NACTVET mwaka 2020.
Akifungua kikao cha wadau Juni 27, 2025 mkoani Tabora, Mwenyekiti wa kikao cha wadau cha kuhuisha mitaala ya chuo cha Ardhi Tabora Bw. Paulo Kitosi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, ushiriki wa wadau kutoa maoni, ushauri na mapendekezo ni muhimu kwa chuo hicho kupata mitaala inayoendana na maendeleo na ukuaji wa ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknoloji.
Kwa mujibu wa miongozo ya NACTVET, mtaala ukiandaliwa huwa na uhai wa miaka mitano na baadaye kuhuishwa ili kukidhi mabadiliko ya uhitaji wa soko ambapo mitaala mitatu ya ARITA imetumika kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2020 na muda wa uhai wake umeisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Bw. Nehemia Minja amesema, chuo hicho kinatoa mafunzo ya kwa ngazi ya Astashahada ya Awali, (NTA Level 4), Astashahada (NTA Level 5) na Astashahada ya Kawaida (NTA Level 6) na kuongeza kuwa kikao hicho kitasaidia kuboresha mitaala hiyo ili kuwaandaa vizuri wanafunzi wa chuo hicho.
Naye Meneja wa NACTVET Kanda ya Magharibi Bi. Faraja Makafu ameeleza kuwa, lengo la ARITA la kuboresha namna ya kuandaa wahitimu wao linaenda kutimia kwa kuwa wamehusisha wadau mbalimbali na kupata maoni yao kulingana na mapungufu waliyoyaona wakati wanatekeleza majukumu yao.