Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kuendelea kusimamia vyema na kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ili halmashauri hiyo iweze kufikia au kuvuka lengo. Amesema mapato hayo ndiyo yanaiwezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza Juni 20, 2025, mara baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same katika kikao kilichojadili taarifa na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Nzowa alisema kuwa mapato hayo ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya wananchi.
Amesema: “Kikubwa ni kuongeza nguvu na juhudi ili makusanyo ya mapato yaweze kufikia lengo, na ikiwezekana kuvuka lengo, kwa sababu makusanyo hayo ndiyo yanayoisaidia serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi. Kadri mapato yanavyozidi kuongezeka, ndivyo serikali inavyopata nguvu zaidi ya kuwahudumia wananchi wake.”
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa kuendelea kupata hati safi, huku akiwahimiza madiwani waliomaliza muda wao kuwa mabalozi wazuri wa kuisemea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewasisitiza madiwani hao kuendelea kushirikiana na serikali kwa kutoa ushauri kwenye kata zao ili kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Vilevile, amewataka wakuu wa idara kuendelea kumshauri kwa weledi Mkurugenzi wa Halmashauri kwa maslahi mapana ya wananchi.
Aidha, Mhe. Kasilda amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Ndg. Jimson Mhagama, kuhakikisha anatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ikiwemo kutokuanzisha miradi mipya wakati ambapo hakuna baraza la madiwani.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Yusto Mapande, amewashukuru madiwani wote waliomaliza muda wao kwa ushirikiano waliouonesha, huku akiwahimiza kuendelea kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali na kijamii.
Amesisitiza pia umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kupokelewa Juni 30, 2025, katika Wilaya ya Same.